NA TEGEMEO KASTUS
Zoezi la kuhakiki mipaka ya hifadhi ya ziwa Manyara na kijiji cha Buger ni maelekezo ya serikali yaliyofikiwa baada ya kikao kilichohusisha mawaziri tisa kutoa mapendekezo. Uhakiki utakuwa shirikishiki kwa kuhusisha wawakilishi wa wananchi wa kawaida, wawakilishi wa serikali ya kijiji, wataalamu wa Halmashauri, wataalamu wa tume ya mipango bora ya ardhi na kutakuwa na wawakilishi wahifadhi wa ziwa Manyara na uhakiki utafanyika kwa kutumia tangazo la gazeti la serikali na kwa kutumia vipimo vya technolojia ya kisasa GPS.
Hayo yamesemwa na Mkuu wa wilaya ya Karatu Mh. Abbas Kayanda kabla ya taarifa za uteuzi, katika mkutano wa hadhara uliofanyika katika kijiji cha Ayalaliyo. Amesema zoezi la uhakiki wa mipaka litahusisha kijiji cha Endonyawet baada ya kumaliza kuhakiki katika kijiji cha Buger na maeneo yaliyowekewa kipaombele katika kijiji hicho kama kitongoji cha Gahabiye, Ayabea Ants-Gamdi na Ayalabe. Amesema zoezi la kuhakiki mipaka ya hifadhi ya ziwa manyara halihusiani kuondoa watu. Amesema wananchi hawapaswi kutaharuki juu ya zoezi hilo, baada ya kuhakiki taarifa itapelekwa serikalini, kama kutakuwa na jambo jingine serikali itatoa taarifa. Amesema uhakiki huo utasaidia kujua mipaka halisi ya eneo la ardhi ya hifadhi ya ziwa Manyara. Amesema kwa sasa kuna mipaka ya mawe matatu jambo ambalo linaleta mkanganyiko kwa wananchi kufahamu mpaka halisi wa hifadhi.
Mh. Abbas Kayanda akizungumza na viongozi wa kata ya buger katika mkutano wa hadhara
Mh. Kayanda amesema wananchi wa Buger wanapaswa kujenga uhusiano mwema na hifadhi ya ziwa Manyara badala ya kujenga mahusiano ya kuvutana. Wananchi wa Buger mnapaswa mumsumbue diwani wenu kuhusu ujenzi wa miradi ya maendeleo. Maendeleo hayawezi kupelekwa sehemu ambayo kila siku watu wanazozana; ameongeza kusema mwaka ujao wa fedha kata ya Buger kuna ujenzi wa kituo cha afya chenye thamani ya million 400 kwa fedha za mapato ya ndani ya Halmashauri, wananchi wanapaswa kujadili na kuweka mkakati juu ya ujenzi wa kituo hicho cha afya.
Amesema ujenzi wa kituo cha afya utasaidia wananchi wa Buger kutotembea umbali mrefu kufuata huduma za afya katika kata ya Endabash. Amesema kata ya Buger imekuwa nyuma kimaendeleo kwa sababu ya migogoro na hilo sio jambo jema. Ni wakati sasa wa kumuunga mkono diwani wenu ili kuchochea maendeleo katika kata ya Buger.
Diwani wa kata ya Buger Mh. Bsili Gitilo akizungumza na wananchi katika mkutano wa hadhara
Naye mwenyekiti wa Halmashauri Mh. John Lucian amesema ili kujenga mawasiliano mazuri na Hifadhi ya ziwa Manyara, ataweka utaratibu wa kuwa na muwakilishi wa Tanapa katika vikao vya baraza la madiwani. Hiyo itasaidia kuimarisha mawasiliano ya moja kwa moja kati hifadhi ya ziwa Manyara na wananchi.
Amesema katika kuleta uelewa wa pamoja elimu zaidi ya ujirani mwema inahitajika kwa wananchi, serikali za Halmashauri za vijiji zitoe mwaliko katika mkutano mkuu wa Halmashauri ya kijiji kwa Tanapa ili kuja kuelimisha wananchi juu ya umuhimu wa kuwa na mahusiano mema na kuzidi kushirikiana. Jitihada hizo za kuelimisha kuhusu ujirani mwema ziende katika vikao vya maendeleo vya kata ili kujenga jamii yenye muitikio chanya juu ya maeneo yaliyotengwa na serikali kwa ajili ya hifadhi.
wananchi wa kata ya Buger wakiwa katika mkutano wa hadhara ofisi ya mtendaji kata
Katika mkutano huo diwani wa Buger Mh. Basili Gitilo amesema mahusiano mabaya katika ya wananchi na hifadhi ya ziwa Manyara imesababisha kasi ya maendeleo katika kata ya Buger kufifia. Amesema ni vyema wananchi kufuata utaratibu na kuelewa sheria za hifadhi ili kujiepusha na vitendo visivyofaa vinavyofanywa na watu wachache ambavyo vinaharibu mahusiano ya jamii nzima ya watu wanaoishi katika kata ya Buger. Amesema kulikuwa na ujenzi wa soko la wanawake ambalo lilipaswa kujengwa na hifadhi ya ziwa Manyara katika kijiji cha Buger lakini kutokana kuvutana vutana na hifadhi soko hilo halijajengwa mpaka sasa.
Mhifadhi Mkuu wa Tanapa Bi, Noelia Myonga akizungumza wakati wa kikao
Mhifadhi Mkuu wa Tanapa Bi, Noelia Myonga amesema katika maisha huwezi kuchagua jirani, amesema ni vigumu sana watu wanaovutana mara kwa mara kukaa na kuzungumza mambo ya maendeleo. Amesema katika kujenga soko la wanawake mradi ulikwama kwa sababu wananchi walishindwa kuweka 30% ya kuchangia soko hilo, hivyo mamlaka kushindwa kuanza kutekeleza mradi, hata hivyo mradi huo bado utafanyiwa kazi. amesema andiko linafanyiwa mapitio na mhandisi wa Halmashauri ili kujua kwa sasa soko hilo linaweza kujengwa kwa kiasi gani cha fedha.
Karatu District Council
Sanduku la Posta: P.O Box 190
Simu: +255 272970648
Simu ya Mkononi: 0754773947
Barua Pepe: ded@karatudc.go.tz
Haki Miliki @ 2017 Halmashauri ya Wilaya ya Karatu.Haki zote zimehifadhiwa