NA TEGEMEO KASTUS
Wananchi wahamasishwa kujenga vyoo bora ili kuepuka magonjwa ya mlipuko yanayotokana na uchafu wa mazingira. Huku mkazo mkubwa ukiwekwa katika kutoa elimu kwa wananchi juu ya umuhimu wa vyoo bora, na matumizi sahihi ya vyoo. Ikiwa ni pamoja na kuhakikisha hatua stahiki zinachukuliwa na viongozi katika kuhimiza wananchi kujenga vyoo bora.
Hayo yamesemwa na Mkuu wa wilaya ya Karatu Mh. Abbas Kayanda wakati akifungua semina ya ukusanyaji wa takwimu za usafi wa Mazingira, iliyohudhuriwa na wenyeviti wa vijiji, watendaji wa vijiji , na watendaji wa Kata katika ukumbi wa ofisi ya Afisa Tarafa Karatu. Ameongeza kusema hakuna mbadala wa afya ndio maana katika seikali za vijiji kuna kamati ya kudumu ya huduma za jamii ambayo ndani yake kuna maswala ya afya na moja ya jukumu lake ni kusimamia na kuhimiza usafi kwa wananchi.
Mh. Abbas Kayanda akizungumza wakati wa ufunguzi wa semina ya mazingira
Akizungumzia kuhusu upatikanaji wa takwimu sahihi za familia zenye vyoo bora, amesema wenyevitii wa vitongoji watakuwa wanawasilisha taarifa kila tarehe 25 ya kila mwisho wa mwezi kwa ofisi ya mtendaji wa kijiji ili aweze kuziandaa na kuwasilisha taarifa hizo kwa mtendaji wa kata. Amesema taarifa hizi za takwimu h zitakuwa zinakusanywa na kutolewa taarifa kwa Mkurugenzi mtendaji wa Halmashauri kabla ya ya tarehe 5 ya mwezi unaoanza. Amesema bado takwimu zinaonesha familia nyingi zina vyoo vya asili, amesema katika takwimu hizo ni kata ya Karatu pekee ndio ambayo haina takwimu za watu wasio na vyoo.
matukio katika picha wakati wa uzinduzi wa semina ya usafi wa mazingira kwa wenyeviti na watendaji wa vijiji na kata
Amesema zoezi la ukusanyaji wa takwimu sahihi za vyoo litakuwa endelevu ili kuweza kupata tathimini ya wapi tumetoka ?? na tunaenda wapi, ametoa wito kwa viongozi wa Karatu kufanya zoezi hilo kwa ukamilifu wake, istokee watu wakatoa takwimu za kupika. Amesema anajua kazi kubwa wanazozifanya watendaji katika kusaidia usimamizi wa miradi ya maendeleo. Kampeni ya usafi wa mazingira iliyofanywa awali imeleta matokeo mazuri na lengo ni kujenga jamii yenye afya bora.
Amesema kuna kaya 219 kwa takwimu za sasa zisizo na vyoo, amesema katika uhamasishaji ulioofanywa tarehe 21, Desember 2018 kwa siku tisa jumla ya kaya 404 hazikuwa na vyoo. Mwaka 2019 kaya zikapungua na kufikia 155 ambazo hazikuwa na vyoo na mwaka 2020 kaya zikaongezeka na kufikia 274 ambazo hazikuwa na vyoo. Lazima tuendelee na msukumo wa kuhimiza wananchi kujenga vyoo bora. Ile kampeni tuliyoianza lazima tuiwekee mwendelezo mzuri wa ufuatiliaji.
Matukio katika picha wakati wa uzinduzi wa semina ya usafi wa Mazingira
Wananchi wanapaswa wajenge vyoo bora na sio bora vyoo, bado watendaji wanakazi kubwa sana ya kufanya katika kuboresha mazingira ya usafi. Majukumu ya viongozi ni pamoja na kutembelea taasisi zilizopo kwenye maeneo ya utawala kwa kufuatilia hali ya usafi wa mazingira ya taasisi hizo. Hakuna mbadala wa afya, lazima wananchi wawe na afya njema ili waweze kujikita katika shughuli za uzalishaji mali. Swala la afya linapaswa kuwa ajenda ya kudumu katika vikao vyetu.
Naye kaimu Mkurugenzi Ndg. Godfrey Luguma amesema katika kampeni ya usafi wa mazingira ni vyema tukazingatia maelekezo ya wataalamu juu ya namna bora ya kukabiliana nayo. Ametoa rai kwa kila mwananchi kuwajibika katika eneo lake kwa kuweka mazingira safi, maeneo yetu tunayafahamu, amesema ikishakuwa kampeni kunakuwa mashindano na nilazima tufanye vizuri ili nasisi tuibuke vinara wa usafi kiwilaya.
Karatu District Council
Sanduku la Posta: P.O Box 190
Simu: +255 272970648
Simu ya Mkononi: 0754773947
Barua Pepe: ded@karatudc.go.tz
Haki Miliki @ 2017 Halmashauri ya Wilaya ya Karatu.Haki zote zimehifadhiwa