Na Tegemeo Kastus
Mkuu wa wilaya ya Karatu Mhe. Theresia Mahongo pamoja na wajumbe wa kamati ya ulinzi na usalama wa wilaya wamefanya ukaguzi wa kushitukiza kwenye maduka ya dawa za binadamu.
Mhe. Theresia Mahongo amesema wamekagua maduka ya dawa za binadamu baada ya taarifa za wasamaria wema waliotilia mashaka uhalali na uwepo wa maduka hayo. Amesema wamebaini wafanyabishara kufanya biashara bila kuwa na kibali, lakini pia wahudumiaji kutokuwa na taaluma ya madawa kama takwa la kisheria linavyotaka. Ukaguzi huo wa kushitukiza ulibaini baadhi ya wafanyabishara wa kawaida kuchanganya biashara, duka moja kuuza vyakula na vileo kwa pamoja jambo ambalo sisawa. Utoaji wa leseni za biashara umetengwa, leseni ya vileo na maduka ya vyakula umetofautiana utoaji wake.
Mhe. Mahongo amesema duka la kwanza la dawa za binadamu walilolitilia shaka linaitwa Reoboth Medic, duka ambalo lipo Mtaa wa ccm Karatu mjini. Amesema Muuzaji wa duka hilo Bi, Jean Bizimana amekiri kwamba yeye ni raia wa Rwanda. Hana taaluma ya ufamasia bali anatumia uzoefu kufanya kazi. Amesema duka la pili limegundulika maeneo ya mtaa wa Fao mjini Karatu, Katika duka hilo wamebaini makasha ya dawa yaliyokuwa yamepangwa kwa ustadi na unadhifu mkubwa huku yakiwa tupu na makasha yaliyokutwa na dawa ni tembe chache zilizokuwa zimebaki.
Mhe. Mahongo amesema vyombo vya ulinzi na usalama vitafanya uchunguzi wa kina ili kubaini kama kuna shughuli nyingine zilizokuwa zinafanyika katika eneo hilo. Amesema muuzaji wa duka hilo ndugu Zakaria Panga miaka (52) anauzoefu wa kuuza kwenye duka la dawa zamani lakini hana vyeti vya ufamasia.
Mhe. Mahongo amesema kwa wale wote wenye maduka ya madawa ya binadamu, kazi ndio imeanza atapitia kukagua wafanyabiashara ili kubaini wafanyabiashara wenye leseni na wasio na leseni. Amesema amepitia maduka ya kawaida ya biashara na amekuta wafanyabishara wa pembezoni wakiwa wanafanya biashara bila kuwa na leseni kwa muda mrefu.
Baadhi ya dawa ambazo zimekutwa katika maduka hayo ya madawa na hazikustahili kuwepo
Mhe. Mahongo amesema Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Karatu anahaja ya kujitafakari kuhusu uwezo na utendaji wa Afisa Biashara kwa udhaifu wa ufuatiliaji ulijitokeza kwenye mapato na leseni za biashara. Ameongeza kusema Mhe. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt, John Pombe Magufuli anapambana na mapato sana, amesema ofisi ya Mkuu wa wilaya imeunda kikosi kazi (Task Force) kufuatilia mapato ili kusaidiana na Halmashauri. Ametoa maelekezo kwa Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri kukagua kila duka mlango kwa mlango ili kujua nani hajalipia leseni ya kufanya biashara.
Mhe. Mahongo amesema kiwanda cha G-Arusha kimekosa fedha za kukimalizia, kama ufutiliaji wa kina utafanyika mapato ya kutekeleza miradi yatapatikana. Amesema watumishi wa Halmashauri waliopewa dhamana ya kufanya kazi wafanye kazi kwa bidii. Ameongeza kusema utendaji kazi wa Afisa biashara siyo mzuri, na matukio ya ukwepaji wa kulipia leseni kwa kiasi hiki umeonesha mapungufu makubwa ya ufuatiliaji.
Mganga Mkuu wa Wilaya Dkt.Mustafa Waziri akiandika maandishi Mekundu ukutani kwenye duka la dawa bubu.
Naye Mganga Mkuu wa wilaya Dkt. Mustafa Waziri ambaye alishiriki katika zoezi hilo amesema ili mtu apate kibali cha kufungua duka la dawa, anapaswa kukaguliwa ili wataalamu wajiridhishe na utoaji wa huduma za dawa. Mfanyabiashara wa duka la dawa anapaswa kuomba kibali kwa Mganga mkuu wa wilaya, na moja ya vigezo vinavyozingatiwa ni pamoja na umbali wa duka moja la dawa na duka jingine uwe unazidi mita 100 au zaidi. Lazima muuzaji awe na hati ya umiliki wa duka lenyewe la dawa na mfanyakazi wa duka la dawa anapaswa kuwa amesomea taaluma ya ufamasia. Amesema kitendo cha kuuza duka la dawa bila kuwa na taaluma ya ufamasia ni hatare sana, ni dhahiri maduka hayo yamefunguliwa kiholela.
Amesema makosa ya aina hiyo kwa watu wanaotumiwa kutenda wanapaswa kwanza kulipa faini ya kiasi cha 500,000.00 ama zaidi au kifungo miezi sita au mwaka mmoja. Amesema Utaratibu ni kwamba maduka yaliyobainika kukiuka masharti ni lazima yafungwe na kuchukua dawa zote na watuhumiwa wapelekwe kituo cha polisi.
Mmoja wa watuhumiwa Bi, Jean Bizimana amesema ameshitimu elimu ya sekondari kidato cha sita huko Kigoma na alichukua mchepuo wa MPC. Amesema mwajiri wake ndiye aliyemuelekeza majina ya dawa na kuanza kuuza duka hilo la madawa ya binadamu. Amesema mpaka sasa ana miezi mitano tangu aanze kufanya kazi.
Karatu District Council
Sanduku la Posta: P.O Box 190
Simu: +255 272970648
Simu ya Mkononi: 0754773947
Barua Pepe: ded@karatudc.go.tz
Haki Miliki @ 2017 Halmashauri ya Wilaya ya Karatu.Haki zote zimehifadhiwa