Na Tegemeo Kastus
Watendaji wa serikali watakaobainika kutumia fedha za makusanyo ya wananchi kinyume na utaratibu watazirejesha fedha hizo. Serikali imekuwa ikisisitiza kusomwa kwa mapato na matumizi ili kujenga uwazi wa fedha zinazokusanywa kwa wananchi na kuziweka katika akaunti husika ya serikali za kijiji ili kuepusha mianya ya ubadhilifu.
Hayo yamebainika baada ya Mlinzi wa zahanati ya Gongali, kumlalamikia Mkuu wa wilaya Mh. Abbas Kayanda akidai kijiji kushindwa kumlipa Mshahara wake kwa wakati na kusababisha malimbikizo ya Madeni ya muda mrefu. Hali iliyolazimisha uongozi wa serikali ya kijiji kumpa kwa kumkodisha shamba la kijiji kiasi cha hekari tatu ili kupunguza deni analodai.
Mh. Dastan Panga katika kikao cha kutatua kero za wananchi.
Mh. Kayanda amesema kuna fedha kiasi cha zaidi ya million tano zilizochangwa na wananchi ambazo hazina uwazi wa mapato na matumizi yake. Fedha ambazo kama zingekuwa zimehifadhiwa benki, ingekuwa ni rahisi kwa uongozi wa serikali ya kijiji kumlipa mlinzi wa zahanati pamoja na mlinzi wa ofisi ya kijiji cha Gongali. Mh. Kayanda ameelekeza taasisi ya kuzuia na kupambana na rushwa kufanya uchunguzi ili kujiridhisha namna fedha hizo zilivyotumika. Kiongozi yeyote wa kijiji atakayebainika kuhusika na ubadhilifu arejeshe fedha hizo na hatua za kinidhamu zichukuliwe dhidi yake.
Mh. Kayanda amesema kijiji cha Gongali kimekuwa na mvutano mkubwa kati ya viongozi wa kitongoji na viongozi wa kijiji, jambo ambalo limesababisha shughuli za maendeleo kudorora. Mh. Kayanda ameelekeza viongozi wa kijiji cha Gongali kuhakikisha wanamaliza tofauti zao za kiuongozi kwa sababu mvutano huo unaumiza wananchi. Ameongeza kusema tabia za watendaji wachache kufanya ubadhilifu ndio zinazopaka madoa serikali mbele ya wananchi hivyo kufanya wananchi kutokuwa na imani na serikali ya kijiji.
Mh. Abbas Kayanda akiwa katika kikao cha kutatua kero za wananchi kijiji cha Gongali.
Katika hatua nyingine Mh. Kayanda ametoa maelekezo mahususi kwa viongozi wa vitongoji kuacha kujihusisha na kuuza ardhi ya kijiji na badala yake uuzaji wa ardhi ufanywe na serikali ya kijiji ili iweze kupata mapato kama sheria za nchi zinavyotaka. Amesema kumekuwa na ujanja ujanja unaofanywa na viongozi wa vitongoji ya kuuza ardhi kiholela jambo ambalo linanyima kijiji asilimia kumi ya mapato yanayotokana na uuzaji wa ardhi. Amesema sheria za ardhi zinaeleza wazi kwamba ardhi ya kijiji ni mali ya kijiji, hivyo mtendaji wa kijiji na mwenyekiti wa kijiji wanachukua dhamana (madaraka) ya kuidhinisha maafikiano ya uuzaji wa ardhi kulingana na makubaliano yatayokuwa yameafikiwa kati ya mnunuzi na muuzaji kulingana na mipango ya ardhi ya kijiji husika.
Mh. Kayanda amekemea vikali tabia za viongozi wa kijiji kutoza fedha wananchi wenye malalamiko ya ardhi, kufanya hivyo ni kuonea wananchi. Ameongeza kusema uongozi ni dhamana, kama umeomba uongozi ina maana ulikuwa umejitoa kuwatumikia watu na sikuwanyonya au kuwakandamiza watu. Amesema kiongozi lazima afanye kazi kwa mujibu wa kiapo chake wakati anakabidhiwa madaraka ya kuongoza.
Picha katika matukio tofauti wakati wa kusikiliza na kutatua kero za wananchi
Karatu District Council
Sanduku la Posta: P.O Box 190
Simu: +255 272970648
Simu ya Mkononi: 0754773947
Barua Pepe: ded@karatudc.go.tz
Haki Miliki @ 2017 Halmashauri ya Wilaya ya Karatu.Haki zote zimehifadhiwa