NA TEGEMEO KASTUS
Usajili wa watoto chini ya miaka mitano wa kuwapa vyeti vya kuzaliwa unaofanya na rita unafanyika bure. Usajili huu wa watoto wenye umri wa chini ya miaka mitano utawawezesha watoto, kupata utambulisho utakaowasaidia kupata huduma nyingine za kijamii. Viongozi katika ngazi mbalimbali wamehimizwa kuhamasisha wananchi kujitokeza kwa wingi kupeleka watoto kujisajili.
Hayo yamesemwa na Mkuu wa wilaya ya Karatu Mh. Abbas Kayanda wakati wa ufunguzi wa zoezi la usajili watoto wenye umri chini ya miaka mitano. Uzinduzi uliofanyika katika uwanja wa mazingira bora wilayani Karatu. Amesema usajili huo kwa sasa unahusisha mikoa ya Arusha na Manyara na utafanywa kwa ushindani ngazi ya mkoa ,ngazi ya wilaya, ngazi ngazi ya tarafara, ngazi ya kata na ngazi ya kijiji. Mh. Kayanda ametoa wito kwa viongozi wa dini katika nyumba za ibada kutoa elimu juu ya umuhimu wa zoezi hili ili wananchi wajitokeze kuandikisha na kusajili watoto walio chini ya umri wa miaka mitano ili wapate vyeti vya kuzaliwa.
Mh. Abbas Kayanda (kulia) akikabidhi cheti cha kuzaliwa kwa mzazi baada ya mtoto kumaliza kusajiliwa
Mh. Kayanda amesema mzazi anapompeleka mtoto kuandikishwa shule, mzazi anapaswa kuwa na cheti cha kuzaliwa cha mtoto. Hali kadhalika mtoto akiingia elimu ya sekondari cheti cha kuzaliwa kinahitajika na akiomba kujiunga na elimu ya juu katika maombi lazima ambatanishe na cheti cha kuzaliwa. Cheti cha kuzaliwa ni muhimu sana kwa watoto wetu, vijana wanaomba kuijunga na jeshi la kujenga taifa katika nyaraka wanazo paswa kuwa nazo ni pamoja na cheti cha kuzaliwa.
Serikali imekuja na kampeni maalumu ya kusajili watoto wenye umri chini ya miaka mitano, ili kuhamasisha wananchi kuwa na vyeti vya kuzaliwa amesema mathalani wilaya ya Karatu ina watu wenye vyeti vya kuzaliwa 14.4% kati ya wakazi 275312. Amesema kwa takwimu hizo ni watu wachache sana wenye vyeti vya kuzaliwa. Ameomba wananchi kuhakikisha wanapata vyeti vya kuzaliwa ili viwe msaada katika huduma nyingine zinazolazimu kuwa na cheti cha kuzaliwa.
Mh. Kayanda ameelekeza waandikishaji katika zoezi hilo kuweka kipao mbele kwa wazee watakaokuja na wajukuu au wakinamama wajawazito watakokuja kuwaandikisha watoto wao wadogo wenye umri wa chini ya miaka mitano. Ametoa rai kwa waandikishaji kufanya kazi kwa uangalifu na kwa kuzingatia mafunzo waliyopata. Amesema hatarajii kuona kuna urasimu katika zoezi la uandikishaji wa watoto wenye umri wa miaka mitano.
shughuli za uandikishaji zikiendelea katika siku ya kwanza ya ufunguzi wa zoezi
Naye Mkurugenzi Mtendaji Ndg.Waziri Mourice amesema serikali imefanya hivi ili kutoa kipaombele kwa wazazi kupata vyeti vya kuzaliwa vya watoto wao. Amewaomba wananchi kuwa mabalozi kwa wengine, kwa kuanzia zoezi litafanyika kwa muda wa siku 14 katika vituo tiba vyote vya serikali na binafsi na katika ofisi za watendaji kata. Amesema na baade zoezi hilo litaendelea tena kwa muda wasiku 90 amesema kwa maandalizi yaliyofanywa katika wilaya ya Karatu wanatarajia kufanya kazi vizuri katika uandikishaji na usajili wa watoto wenye umri chini ya miaka mitano.
Karatu District Council
Sanduku la Posta: P.O Box 190
Simu: +255 272970648
Simu ya Mkononi: 0754773947
Barua Pepe: ded@karatudc.go.tz
Haki Miliki @ 2017 Halmashauri ya Wilaya ya Karatu.Haki zote zimehifadhiwa