Na Tegemeo Kastus
Wito umetolewa kwa viongozi kuhamasisha wananchi kujiunga na mfuko wa bima ya afya iliyoboreshwa, manufaa ya bima ya afya iliyoboreshwa ni kusaidia wananchi kupata matibabu bila kuwa na hofu ya gharama za matibabu. Bima hiyo inatolewa kwa kiasi cha shilingi elfu thelathini kwa kaya ikijumuisha watu sita kwa kipindi cha mwaka.
Mh. Kayanda akizungumza katika baraza la madiwani
Hayo yamesemwa na Mkuu wa wilaya ya Karatu Mh. Abbas kayanda alipokuwa akizungumza katika kikao cha baraza la madiwani kilichofanyika katika ukumbi wa Halmashauri kilichokuwa kikirushwa mubashara (kwa matangazo ya moja kwa moja) na kituo cha redio Lumen. Mh. Kayanda ametoa wito kwa Madiwani na Wenyeviti kuhamasisha wananchi kujiunga na Ichf iliyoboreshwa. Amesema muitikio kwa sasa bado ni mdogo kaya zilizojiandikisha na Ichf iliyoboreshwa ni 2695 ambayo ni sawa na 6%.
Sambamba na hilo Mh. Kayanda ameelekeza baraza kupitia kwa Mwenyekiti wa Halmashuri kulipa deni la shilingi million 3 inalodaiwa, ili kuweza kupata vifaa na kuongeza kasi uandikishaji wananchi katika mfuko wa bima ya afya. Ameongeza kusema kuna wadau wa maendeleo wamejitokeza kusaidia kaya 324 kujiandikisha na Ichf iliyoboreshwa. Ametoa rai kwa watendaji wa serikali kujipanga ili kuongeza kasi ya uandikishaji wa bima ya afya iliyoboreshwa.
Matukio katika picha wakati wa baraza la madiwani
Akizungumzia sekta ya barabara Mh. Kayanda amesema serikali ya awamu ya sita kupitia Rais, Mh. Samia Suluhu Hasani imetoa kiasi cha Billion 2.5 wakala wa barabara vijijini. Fedha zinazotarajiwa kufungua barabara, na kutengeneza barabara mbalimbali za katika Halmashauri ya wilaya ya Karatu. Amesema kuna kiasi cha million 500 ambacho kitatumika kuweka lami katika mji wa Karatu kuanzia barabara ya Redstone kuelekea sokoni kuelekea Ttcl mpaka camp david.
Amesema serikali kupitia Ruwasa imetoa fedha kwa ajili ya ujenzi wa miradi ya maji takribani billion 2.2 katika Halmashauri ya wilaya ya Karatu. Amesema katika sekta ya maji kumekuwa na changamoto kubwa katika uendeshaji wa bodi za maji. Amesema serikali imekuja na muundo mpya wa bodi za maji hivyo bodi za sasa zitafumuliwa ili kuweka watu wenye sifa na taaluma zinazoendana na taaluma ya maji, ambao watakuwa tayari kuzitumikia.
Matukio katika picha wakati wa baraza la madiwani
Akizungumzia zoezi la utambuzi wa walengwa wa Tasaf Mh. Kayanda amekemea tabia ya viongozi wa serikali kushindwa kusimamia zoezi hilo kikamilifu hasa katika kijiji cha Mang’ola barazani. Amesema katika kijiji hicho kuna kaya 688 ambazo zinapaswa kuandikishwa, wingi wa kaya hizo unakaribiana na idadi ya jumla ya kaya zote zilizopo katika kijiji cha Mang’ola barazani. Amesema takwimu hizo zinaleta dosari katika utekelezaji wa utambuzi wa kaya za walengwa, amesema zoezi hilo litafanywa kwa maelekezo ya tasaf na si kwa utashi wa mtu binafsi.
Kuhusu usambazaji wa umeme vijijini Mh. Kayanda amesema serikali inaendelea kusambaza umeme wa REA vijijini, baaada ya mkandarasi wa awali kampuni ya NIPO kushindwa. Tanesco kupitia kampuni Tanzu itamalizia viporo vya umeme wa REA awamu ya tatu mzunguko wa kwanza kwa vijiji vyote vilivyokuwa vimebakia kama Gongali, Rhotia Kati, Kainam, Baray Khusumay, Endala Shangit, kilimamoja, Huduma.
Amesema usambazaji wa umeme wa Rea wa awamu ya tatu Mzunguko wa pili utahusisha vijiji vya Matala, Mang,ola juu, Makoromba Endamaghan, Mikocheni Endala. Amesema serikali inalenga kusambaza umeme wa Rea kwa vijiji vyote. Sambamba na hilo Mh. Kayanda amesema serikali inalenga kuimarisha huduma za mawasiliano kwa umma katika maeneo ambayo hayana huduma za mawasiliano. Ametoa wito kwa viongozi wa kijiji na madiwani kutoa taarifa ya meneo yenye shida ya mawasiliano ili yawekwe kwenye mpango wa serikali tayari kwa kujenga minara ya mawasiliano katika maeneo hayo.
Watendaji wakiwa katika kikao cha baraza la madiwani.
Mwenyekiti wa Halmashauri Mh. John Lucian amesema utekelezaji wa bajeti ya mwaka huu wa fedha umeshaanza, amesema Halmashauri imetenga kiasi cha million 400 katika mapato yake ya ndani kwa ajili ya ujenzi wa kituo cha afya kata ya Buger. Amesema sasa ni wakati wa kuanza kusimamia utekelezaji wa bajeti, ametoa rai kwa viongozi na watendaji kusimamia miradi ya mendeleo kikamilifu. Amesema wananchi wa buger wanasubiri ujenzi wa kituo cha afya kwa shauku kubwa.
Naye mkurugenzi mtendaji wa Halmashauri ya Karatu Ndg. Karia Rajabu amesema katika kusimamia mpango wa bajeti, utoaji wa mikopo kwa vikundi vya kinamama vijana na walemavu itakuwa inatolewa baada ya kupitishwa na kamati ya fedha. Amesema mara baada ya kupitishwa na kamati ya fedha baraza litaizinisha utolewaji wa mikopo amesema utaratibu huo utaondoa malalamiko kwa wananchi juu ya namna ya kupata mikopo hiyo.
Ndg. Rajabu amesema bado wataalamu wa maendeleo ya jamii watatumika kutambua vikundi vya mikopo kupitia kamati maalumu ambayo itatoa mapendekezo kwa kikao cha wataalamu CMT. Ili baada ya hapo mapendekezo yaende kamati ya fedha kwa ajili ya kuhuishwa, amesema utaratibu huu utaleta uwazi juu ya namna ya vikundi vitakavyonufaika na mikopo isiyo na riba ya Halmashauri inavyotolewa.
Matukio katika picha wakati wa kikao cha baraza la madiwani
Karatu District Council
Sanduku la Posta: P.O Box 190
Simu: +255 272970648
Simu ya Mkononi: 0754773947
Barua Pepe: ded@karatudc.go.tz
Haki Miliki @ 2017 Halmashauri ya Wilaya ya Karatu.Haki zote zimehifadhiwa