Na Tegemeo Kastus
Serikali imewataka wananchi wa vijiji vya Qaru na Kinihhe kudumisha umoja na mshikamano ili kuchochea ujenzi wa miradi ya maendeleo. Viongozi mmepewa dhamana ya kuongoza lazima muwe mfano katika kuongoza wananchi kwa kutekeleza maamuzi halali ya vikao vya Halamashauri kuu ya kijiji. Ni jukumu la viongozi kutafuta ufumbuzi wa pamoja kwa njia ya majadiliano na kuridhiana pindi inapotokea utofauti wa kimtazamo katika kuongoza.
Mh. Kayanda akiwa katika kikao cha ndani na wajumbe wa Halmashauri vijiji vya Qaru na Kinihhe
Hayo yamejiri katika kikao cha ndani cha Mkuu wa wilaya ya Karatu Mh. Abbas Kayanda na wajumbe wa Halmashauri ya viijiji vya Qaru na Kinihhe. Katika kikao hicho Mh. Kayanda amesisitiza umuhimu wa viongozi kukaa pamoja na wataalamu wa ardhi ili kukusanya maoni juu ya mvutano wa mpaka kati ya kijiji mama Qaru na kijiji cha kinihhe ufanyike, kupitia vikao vya Halmashauri kuu ya vijiji vya Qaru na Kinihhe. Ili baada ya hapo mapendekezo yapelekwe katika vikao vya maendeleo ya kata kwa ajili ya kupata ufumbuzi wa kudumu.
Kuhusu swala la kugawana mali zilizozalishwa kwa pamoja kabla ya kijiji cha Kinihhe hakijajitenga kutoka kijiji cha Qaru mwaka 2009. Mh. Kayanda ameelekeza viongozi wa serikali ya kijiji cha Kinihhe kuandika barua kwa Mkurugenzi Mtendaji wa Halamashuri ya Karatu na nakala kwenda katibu tawala wa wilaya ya Karatu wakiomba kuundwa kwa kamati ya mgao wa mali ili kuwezesha taratibu za mchakato wa kugawana mali kuanza.
Wajumbe wa serikali za vijiji vya Qaru na Kinihhe kwenye katika kikao cha ndani
Katika mkutano wa hadhara na wananchi wa kijiji cha Kinnhe Mh. Kayanda amehimiza wananchi kuendelea kudumisha mahusiano mazuri na kijiji mama cha Qaru. Amesema mivutano inachelewesha kasi ya ujenzi wa miradi ya maendeleo. Ameelekeza Meneja wa tanesco wilaya ya Karatu, kufanya tathimini kwenye kijiji cha kinihhe kwa ajili ya kukiweka kijiji hicho kwenye mpango wa usambazaji wa umeme vijijini (REA) mwaka ujao wa fedha.
Wakati huo huo Mh. Kayanda amemuelekeza Mganga Mkuu wa wilaya ya Karatu kufanyia tathimini na kuliweka jengo la zahanati ya kijiji cha kinihhe katika mpango wa bajeti ya Halmashauri ili jengo la zahanati hiyo liweze kukamilika na lianze kutoa huduma. Katika hatua nyingine Mh. Kayanda ameelekeza wataalamu wa ardhi wa wilaya kwenda kupima eneo la chanzo cha maji kinachohudumia vijiji vya Qaru na Kinihhe, ili kujua ukubwa wake halisi baada ya kuwepo taarifa kuwa eneo hilo limevamiwa na shughuli za kibinadamu zinafanywa ndani ya chanzo cha maji. Amesema kufanya shughuli za kibinadamu kwenye eneo la chanzo cha maji kisheria ni makosa. Amemuelekeza Afisa tarafa wa Endabash kwenda kulitembelea eneo hilo la chanzo cha maji na kulitolea taarifa ofisi ya mkuu wa wilaya.
Mwenyekiti Ndg. Vicent Gabriel akifungua Mkutano wa hadhara
Akizungumzia kuhusu swala la wanafunzi kupata chakula shuleni, Mh. Kayanda amesema mpango huo ni mzuri na unalenga kuboresha maendeleo ya kitaaluma. Amesema kama vikao vya Halmashauri ya vijiji vilikaa na kukubaliana wazazi wachangie chakula cha wanafunzi shuleni basi serikali za vijiji hazina budi kusimamia maamuzi halali ya vikao vya Halmashuri ya kijiji. Amesema serikali ya kijiji cha Qaru ikae na iweke msukumo kwa wanafunzi wanaosoma katika shule ya msingi Qarulambo na sekondari ya Qaru wawe wanapata chakula cha mchana shuleni, halikadhalika serikali ya kijiji cha Kinihhe isimamie wazazi wa kijiji hicho ili kuhakikisha wanafunzi wanaosoma shule ya msingi QaruLamabo na sekondari Qaru wawe wanapata chakula cha mchana shuleni.
Awali katika Mkutano wa hadhara Mwenyekiti wa kijiji cha Kinihhe Ndg. Vicent Gabriel alisema kulikuwa na mvutano mkubwa na kijiji mama cha Qaru. Hivyo kusababisha wananchi kususia kujitolea nguvu kazi na michango kwa ajili ya ujenzi wa shule ya sekondari Qaru. Amesema sababu kubwa ni mabishano ya mpaka, amesema wananchi wa Kinihhe walikuwa wananung’unikia kutopewa mgao wa mali kutoka kijiji mama cha Qaru.
Wananchi wa kijiji cha Kinihhe wakiwa katika mkutano wa hadhara
Ndg. Gabriele amesema hata kijiji cha Qaru kilikuwa na manung’uniko juu ya kutofautiana kuhusu mipaka halisi ya inayotenganisha vijiji vya Qaru na Kinihhe. amesema maelekezo ya Mkuu wa wilaya yameleta usawa na kuondoa malalamiko ya muda mrefu yaliyokuwa yanazorotesha maendeleo katika kijiji cha Kinihhe na kijiji cha Qaru. Amesema sasa wamefungua ukurasa mpya na wameweka tofauti zao pembeni. Ndg. Gabriel amehimiza swala la wananchi kujitoa nguvu kazi katika kuchangia ujenzi wa miradi ya maendeleo. Amesema wajumbe wa Halmashuri ya kijiji cha Kinihhe wanatakiwa kukamilisha mchango wa 36000 itakapofika 20/9/2021 kwa ajili ya ujenzi wa vyumba vya madarasa katika shule ya sekondari Qaru kama walivyokubaliana katika vikao vya Halmashauri ya kijiji huku wananchi wa kijiji hicho wakitakiwa kukamilisha mchango wa kuchangia ujenzi wa vyumba vya madarasa ifikapo tarehe 20/10/2021. Amesema kijiji cha Qaru kimefika katika hatua nzuri katika kuchangia ujenzi wa vyumba vya madarasa katika shule ya sekondari Qaru. Ujenzi wa vyumba vya madarasa ni jitihada za serikali za vijiji vyote viwili katika kukabiliana na changamoto ya upungufu wa madarasa katika shule ya sekondari Qaru inayotarajia kupokea mwakani, makisio ya wanafunzi 190 wa kidato cha kwanza kutoka kwenye vijiji vya Qaru na Kinihhe.
Mh. Kayanda akikagua jengo la zahanati ya Kinihhe
Karatu District Council
Sanduku la Posta: P.O Box 190
Simu: +255 272970648
Simu ya Mkononi: 0754773947
Barua Pepe: ded@karatudc.go.tz
Haki Miliki @ 2017 Halmashauri ya Wilaya ya Karatu.Haki zote zimehifadhiwa