Mafunzo kwa viongozi wa serikali wilaya ya Karatu yamefanyika katika ukumbi wa Halmashauri. Mafunzo hayo ya siku moja yalilenga kuhimiza viongozi kufanya kazi kwa kufuata sheria na maadili ya viongozi wa umma, kwa kufanya kazi kwa uadilifu upole na kwa njia inayokuza imani ya wananchi katika utekelezaji wa shughuli za umma.
Mhe. Theresia Mahongo amesema anapokea malalamiko mengi sana kwa wananchi katika idara ya ardhi, amesema mara nyingi hawapo ofisini. Ametoa malekezo kwa watendaji kuwa na mpango kazi ili watu wafahamu siku gani wanakuwepo ofisini na siku gani watendaji wanakuwa nje ya vituo vya kazi. Mhe. Mahongo amesema hayo wakati akifunga semina iliyoongoza na tume ya maadili kanda ya kaskazini kwa viongozi wa wilaya ya karatu iliyolenga kuwajengea uwezo wa kutimiza majukumu yao ya kazi vyema.
wakuu wa idara wakiwa katika semina kwenye ukumbi wa Halmashauri
Mhe. Mahongo amehimiza viongozi kufuata maadili, amesema kuna tabia ya viongozi kutoa taarifa za vikao vya ndani nje ya Ofisi, ambazo mwishowe zinaleta shida kiutendaji. Amesema kutoa taarifa za ndani za vikao kwa watu wa nje zinaleta mpasuko, amehimiza watendaji kuwa na ushirikiano katika utendaji wa shughuli za serikali.
Mhe. Mahongo amehimiza viongozi wa wilaya kuanza kujiamini wenyewe katika kazi zao, amesema hiyo itachangia kufanya kazi kwa ufanisi. Idara itasimama vizuri katika utendaji wa kazi na hiyo itasaidia kuwa kiongozi mzuri. Amesema si idara zote zinafanya vibaya, kuna idara zianafanya vizuri sana, Mhe. Mahongo amesema kuna wilaya zinafanya vizuri upo umuhimu wa kwenda kujifunza namna zinavyofanya kazi. Mhe. Mahongo amesema miradi yote inayofanyika hivi sasa anaisimamia kwa karibu ndio maana miradi iliyoanza tangu 2016 yote inaendana na thamani ya fedha. Mhe. Mahongo ametoa wito kwa idara ya manunuzi Halmashauri ya wilaya ya Karatu kuzingatia maadili katika utendaji wa shughuli zake.
Mhe. Mahongo amempongeza Mhe. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli ambaye ofisi ya Tamisemi ipo chini yake ikiwa inaongozwa Mhe. Jaffo amesema hiyo imesaidia kubadilisha baadhi ya watumishi. Ameomba watumishi kuazimia kufanya kazi bidii, amesema Mkuu wa idara unapaswa kujiwekea mipango mizuri kwa sababu wewe ndio injini, Mkurugenzi ni msimamizi. Amesisisitiza Wakuu wa idara kujipima kulingana na ufanisi wa kazi zao.
Mhe.Mahongo ametoa wito kwa watu wa ustawi kujikita katika kutoa elimu, amesema maadili yameanza kuporomoka katika ngazi ya familia. Amesema mtoto ajengwe vizuri katika ngazi ya familia namna ya kujituma katika kazi vitu hivyo ndio vina vinamjenga kuwa baadae mtumishi mwema wa umma. Mhe. Mahongo amehimiza kwa watumishi kujenga utamaduni wa kutunza siri za ofisi, ametoa maelekezo kila mkuu wa idara kukaa na watumishi wa chini yake na kuwapa elimu juu ya umuhimu wa kuhifadhi siri za ofisi.
Wakuu wa idara wakisikiliza semina iliyokuwa ikitolewa na viongozi wa tume ya maadili
Awali katika mafunzo hayo Katibu msaidizi sekretarieti ya maadili ya viongozi wa umma kanda ya kasikazini Bi, Anna Mbasha amehimiza umuhimu wa viongozi kuwasilisha tamko la rasilimali na madeni. Mafunzo hayo yalilenga kuwapa viongozi wa umma miongozo ya kuepuka migongano ya kimaslahi katika utekelezaji wa shughuli za serikali.
Bi, Mbasha amesema mgongano wa kimaslahi husababisha wananchi kukosa imani na serikali kutokana na miradi ya serikali kutekelezwa chini ya kiwango na kwa manufaa ya wachache. Bi, Mbasha amehimiza kwa viongozi kujitoa katika miradi na kuweka maslahi ya umma mbele pindi wanapothibitisha pasipo na shaka kwamba kuna mradi una mgongano wa kimaslahi.
Afisa sheria Ndugu. Prosper Ndomba amesema mafunzo yaliyotolewa na tume ya maadili yamewapa picha kubwa juu ya mgongano wa kimaslahi. Amesema amejifunza kwamba mgongano wa kimaslahi unaweza ukawepo hata kwa utaratibu wa kufuata kisheria. Amesema mathalani kiongozi katika eneo lake la usimamizi wa kazi; ikitokea mtoto wake akiomba kazi katika eneo hilo hata kama anasifa stahiki litaleta taswira ya mgongano wa kimaslahi, kwa sababu mgongano wa kimaslahi ni jambo la mtizamo wa kihisia.
Ndugu Ndomba Amesema katika mafunzo hayo amejifunza juu ya swala la uzalendo katika utendaji wa shughuli za serikali. Amesema ili kuweza kufanya hivyo lazima kushinda tamaa za moyo katika utendaji wa shughuli za serikali ili kuleta utendaji wenye matokeo chanya.
Karatu District Council
Sanduku la Posta: P.O Box 190
Simu: +255 272970648
Simu ya Mkononi: 0754773947
Barua Pepe: ded@karatudc.go.tz
Haki Miliki @ 2017 Halmashauri ya Wilaya ya Karatu.Haki zote zimehifadhiwa