Na Tegemeo Kastus
Serikali imerejesha ardhi kiasi cha hekari moja iliyokuwa imeporwa kwa njia ya utapeli kwa Mjane Bi, Priska Slaa. Ardhi hiyo imerejeshwa baada ya mlalamikiwa kushindwa kuleta ushahidi wa vielelezo wa umiliki wa ardhi na hivyo kufanya utatuzi wa mgogoro wa ardhi uliofanyika kwa njia za kiutawala kwa muda wa siku tatu kujiridhisha na ushahidi uliotolewa na mlalamikaji kwamba ndiye mmiliki sahihi wa ardhi hiyo.
Mh. Kayanda amesema lazima watu waishi kwa misingi ya utu, karatu kumekuwa na tabia ya kuwaonea sana wakinamama wa jane. Mh. Kayanda amekemea tabia zisizo za kiungwana zinazomea mizizi kwenye jamii. Ameelekeza viongozi wa kijiji na kata kuhakikisha hakuna uvunjifu wa amani utakaotokea baada ya Bi, Priska kupewa eneo lake.
Bi, Prisca Slaa Mjane aliyerejeshewa shamba lililokuwa limechukuliwa kiujanja ujanja
Naye Bi. Priska Slaa ameishukuru serikali kwa kusimamia na kuhakikisha suluhu ya mgogoro wake wa ardhi uliokuwa unamtatiza umeisha. Amesema hii imekuwa faraja kwake na hafikirii tena kukodisha shamba lake kwa mtu na badala yake anafikiria kuliendeleza kwa kufanya shughuli za kilimo au kulipanda miti. Lengo ikiwa ni kukusanya nguvu ili aweze kujenga nyumba katika eneo lake.
Bi. Slaa akisimulia madhila yaliyomkuta amesema alikuwa mtumishi wa serikali ya kijiji cha Bashay ambacho ni kijiji mama kilichozaa kijiji kipya cha Dofa. Anasema wakati huo alikuwa anafanya kazi katika serikali ya kijiji cha Bashay ambayo iliweka utaratibu wa kuwagawia ardhi watumishi wa serikali ya kijiji ambayo ndio aliyokuwa akiipigania. Ili irejee katika umiliki wake na aweze kuitumia kujiongezea kipato.
Bi. Slaa anasema Ndg. Fiita Barbyu Masay alimuomba eneo hilo la shamba amkodishe ili afanye shughuli za kilimo. Baada ya kulima mwaka wa kwanza mwaka uliofuata alilima lakini alidai hakupata mavuno mazuri, malipo ya kukodisha shamba hayakwenda kama walivyokubaliana. Anasema mwaka uliofuta mzee Fiita alimleta mtu mwingine kukodisha shamba na akamuelekeza mwenye shamba ni Bi, Priska Slaa.
Katika hatua za kusikiliza mgogoro huo Ndg. Mwarabu Lohay ambaye ndiye alikuwa akilima shamba hilo kwa kukodi kwa mama huyo amesema shamba alilokuwa akilima alioneshwa na Mzee Fiita Masay ambaye alimuelekeza kwamba Bi, Prisca Slaa ndiye mmiliki wake na katika kipindi chote alichokuwa akilima alikuwa analipa kodi kwa Bi, Prisca Slaa.
Mh. Abbas Kayanda akiwa katika eneo la shamba lenye mgogoro pamoja na mashahidi wa kila upande
Katika sakata hilo Msaidizi wa Mtendaji wa kijiji aliyehusika kugawa ardhi kwa wafanyakazi wa kijiji cha Bashay kabla ya kuzaa kijiji cha Dofa Ndg. Martin Nicodemus pamoja na mzee aliyejitambulisha kwa jina la Gabriel Manoy wamesema wanafahamu namna ardhi hiyo ilivyogawiwa katika kipindi hicho kwa sababu wao ndio walioshikiri kupiga hatua za kulipima ukubwa wa shamba hilo.
Naye mlalamikiwa Ndg. Fiita Masay amesema wazee waliokuwa wanapima ardhi katika eneo hilo alishawapeleka eneo la shamba hilo awali wakati mgogoro wa shamba hilo ukiwa unashughulikiwa katika ngazi ya kijiji lakini walipofika katika eneo la shamba lilogombaniwa walishindwa kuthibitisha kama eneo ni la Bi, Prisca Slaa. Ndg. Fiita anasema amestaajabishwa kwa sababu awamu hii ya utatuzi wa mgogoro wameweza kulihakikisha na wote wamethibitisha kuwa ni eneo la Prisca Slaa.
Ndg. Fiita katika siku zote alizoitwa kusikilizwa shauri lake ameshindwa kuonesha vielelezo vya maandishi kama kweli eneo hilo lenye mgogoro ni lake. Siku ya usikilizaji wa shauri lake alidai vielelezo anavyo mke wake na hakuwa eneo la karibu kwa sababu alikuwa ameenda mnadani kutafuta mahitaji ya nyumbani, lakini anaweza kuvipata vielelezo hivyo baada ya siku mbili. Katika kukamilisha ushahidi wa utetezi wake siku ya mwisho Ndg. Fiita amesema amekwama kuonana na mke wake kwa sababu ambazo hakuziweka wazi hivyo kushindwa kuthibitisha uhalali wake wa umiliki wa eneo hilo la shamba.
Mh. Abbas Kayanda katika matukio tofauti katika eneo lenye mgogoro wa ardhi.
Mh. Dastan Panga diwani wa kata ya Qurus amesema kumekuwa na katabia hasa kwa watu wenye uwezo kuchukua ardhi kwa nguvu. Amesema eneo la ardhi ya Bi. Prisca Slaa lilikuwa limechukuliwa kwa nguvu na Ndg. Fiita ambaye alidiriki kuliuza kwa mtu mwingine aliyefahamika kwa jina moja la Niiman ambaye alikuwa anataka kujenga. Uongozi wa kijiji cha Dofa uliingilia kati swala hilo na kuweka zuio la muda la ujenzi katika eneo hilo mpaka mgogoro huo utakapopatiwa ufumbuzi. Mh. Panga ameshukuru kwa uamuzi uliofanywa na serikali kwa sababu tayari watu wenye uwezo wa kifedha wameshaanza tabia ya kunyang’anya watu wasio na uwezo wa fedha maeneo ya ardhi kwa nguvu.
Karatu District Council
Sanduku la Posta: P.O Box 190
Simu: +255 272970648
Simu ya Mkononi: 0754773947
Barua Pepe: ded@karatudc.go.tz
Haki Miliki @ 2017 Halmashauri ya Wilaya ya Karatu.Haki zote zimehifadhiwa