NA TEGEMEO KASTUS
Wafadhili wa Africa foundation wamekabidhi kwa serikali ujenzi wa bweni la wavulana na jengo la choo cha wasichana vienye thamani ya pamoja zaidi ya million 113 kwa shule ya sekondari kilimamoja. Bweni la wavulana lina uwezo wa kubeba wanafunzi 64 litakuwa msaada kwa wanafunzi wanaotoka mbali na eneo la shule.
Mkuu wa wilaya ya Karatu Mh. Abbas Kayanda amewapongeza wafadhili hao kwa msaada waliotoa kwa shule ya sekondari kilimamoja. Amesema wadau wa elimu kazi wanayofanya ni kuunga mkono kazi kubwa iliyofanywa na Mh. Rais Dkt. John Pombe Magufuli ya kuimarisha miundo mbinu katika shule ya msingi na sekondari. Amesema serikali imetengeneza mazingira mazuri ya uwekezaji na mambo haya wanayoyafanya wawekezaji hawa ni kurudisha shukrani kwa jamii.
Mh. Abbas Kayanda akikagua bweni la wavulana kwa ndani.
Muonekano wa bweni la wavulana kwa nje.
Mh. Kayanda amesema muwekezaji Africa foundation anaamini kabisa njia pekee ya kuikomboa jamii ni kuwekeza katika elimu. Amesema elimu inatoa maarifa ambayo yakiingia kichwani hayawezi kupotea. Amewaasa wanafunzi kusoma kwa bidii ili elimu yao ije kusaidia jamii, amesema ili mwanafunzi aweze kufikia malengo yake lazima awe na nidhamu. Lazima miundo mbinu iliyojengwa ichochee kiwango cha ufaulu wa wanafunzi. Amesema mabadiliko ya kitaaluma ndio yatakayoonyesha umuhimu wa miundo iliyojengwa.
Mh. Kayanda ametoa wito kwa walimu kusimamia na kuhakikisha miundo mbinu inadumu kwa muda mrefu, lakini kuchukua hatua stahiki kwa mtu yeyote atakayeharibu miundo mbinu. Amewaasa wanafunzi kuwa na nidhamu ya matumizi ya miundo mbinu iliyojengwa na kila mwanafunzi kuwa mlinzi wa mwenzake.
Mh. Abbas Kayanda (kulia) akizindua jengo la choo cha wasichana sekondari ya Kilimamoja.
Mh. Abbas Kayanda akikagua jengo la choo cha wasichana sekondari ya Kilimamoja.
Awali Afisa elimu sekondari Bi, Kalista Maina amesema bweni lilojengwa litasaidia wanafunzi kupunguza utoro wa mara kwa mara na vishawishi mbalimbali. Amesema bweni hilo litawaongezea umakini wa kusoma kwa bidii ili waweze kutimiza malengo yao. Amesema bweni litasaidia wanafunzi kupata muda mwingi wa kujisomea wakati wa usiku lakini kuwaondolea wanafunzi uchovu wa kutembea umbali mrefu kutoka nyumbani.Bi.Maina ameomba wazazi kuwajibika kwa watoto wao kwa kuhakikisha wanapatia wanafunzi mahitaji yote muhimu kwa wakati.
Naye Mkurugezni wa Africa Foundation Dkt. Ernest Mgono amesema shule ya sekondari kilimamoja ipo karibu na maeneo ya hifadhi na maeneo hayo ya hifadhi, amesema katika maeneo hayo ya uhifadhi ndipo walipoweka vitega uchumi vyao. Hivyo kwa kuwa katika maeneo waliyowekeza kuna jamii inawazunguka lazima jamii ipate faida kidogo ili waendelee kujali na kutunza hifadhi.
Dkt. Mgono amesema walishaanza kujenga bwalo la chakula lakini wameshajenga bwala la wanafunzi wa kike kabla ya kukabidhi bwalo la wanafunzi wa kiume. Amewaomba wanafunzi kutunza majengo yote yaliyojengwa ili majengo hayo yaweze kudumu kwa muda mrefu.
Karatu District Council
Sanduku la Posta: P.O Box 190
Simu: +255 272970648
Simu ya Mkononi: 0754773947
Barua Pepe: ded@karatudc.go.tz
Haki Miliki @ 2017 Halmashauri ya Wilaya ya Karatu.Haki zote zimehifadhiwa