Kinamama wajasiriamali wa kikundi cha Juhudi na Kujitegemea Wilayani Karatu, wamekuwa mfano kwa vikundi vingine kwa kukuza na kuimarisha mradi wa kuuza maziwa ya ng’ombe. Hayo yamesemwa na Mratibu wa vikundi vya kinamama Bi, Adela Shauri alipokitembelea kikundi hicho mwishoni mwa wiki.
Halmashauri ya wilaya ya Karatu iliwapatia mkopo kinamama hao pamoja na elimu ya ujasiriamali kupitia Idara ya Maendeleo ya Jamii. Mkopo ambao umewasaidia kinamama hao kujikwamua kiuchumi kwa kuongeza wigo wa kipato chao.
Kikundi kilianza katika kijiji cha Gongali lakini kutokana na hitaji la kuwafikia wateja wa maziwa kwa urahisi walihamisha mradi kwenda Karatu mjini. Bi, Martha Panga, ambaye ni Mhasibu wa kikundi hicho anasema kikundi kina jumla ya wanachama kumi walianza mwaka 1995, wakijishughulisha na kufyatua matofali.
Bi, Martha anasema awali walikuwa wanafanya mikutano yao chini ya mti katika kijiji cha Gongali na kukopeshana wenyewe kwa wenyewe. Walianza na shughuli ya kufyatua matofali ambayo ilikuwa ngumu ikawashinda; wakaamua kutengeneza pombe ya kienyeji, ambayo pia iliwashinda kutokana na pombe kuchachuka. Bi Martha anasema waliamua kujishughulisha na kilimo, walilima wakapata mahindi gunia sita na kipindi hicho gunia la mahindi lilikuwa linauzwa shilingi elfu nne. Wakaanza kukopeshana wenyewe kwa muda wa miezi mitatu mpaka sita ili kukuza mtaji na mtu wa kwanza waliyemkopesha walipata elfu arobaini, mtu wa pili wakapata elfu thelathini na mtu wa tatu wakapata elfu kumi kitu ambacho kiliwasaidia kurudisha riba.
Bi Martha anasema Halmashauri ya Wilaya ya Karatu iliwapeleka semina Tengeru walienda kujifunza kuhusu usindikaji na baadae Halmashauri iliwaasaidia kupata elimu ya ujasiriamali na wakafanikiwa kupata mkopo wa million moja na nusu. Bi Martha anasema mkopo huo haukuwa fedha taslimu bali walinunuliwa vifaa kama mashine ambayo ni Cream separator, Makeni, na Masufuria. Bi Martha anasema waliweza kurudisha mkopo kutokana na shughuli zao za kugandisha maziwa walizokuwa wameanza.Wanakikundi walianza kwa kugandisha lita ishirini, baadae lita arobaini, baadae lita hamsini na mpaka sasa wanagandisha lita mia na hamsini.
Bi Beatha Yotham ambaye ni mmoja wa wanachama anasema malengo ya mradi wao ni kuwawezesha kujikwamua kutoka kwenye maisha duni. Bi Beatha anasema wamefanikiwa kununua viawanja vitatu, ambacho kimoja wamenunua million tano, kiwanja kingine Million nane na kiwanja cha tatu walinunua kwa shilingi elfu hamisini. Wameweza kujenga nyumba katika kiwanja kimoja na wamepangisha wapangaji wawili. Lakini pia wamefungua mradi wa pili wa maziwa Stendi ya Karatu unao wagharimu kama million tatu kwa mwaka kama kodi ya pango. Lengo lao ni kuwasogezea wateja wao huduma karibu, lakini pia kutokana na shughuli zao Halmashauri imewapa mkopo tena wa million kumi kwa ajili ya kuboresha shughuli zao.
Bi Beatha anasema changamoto kubwa kwao kwa sasa ni wakati wa kipindi cha baridi ambacho kiasi kikubwa cha maziwa kinabaki bila kununuliwa. Wenyewe kama wanakikundi wanaona wakipata mtungi mkubwa wa kuhifadhia maziwa wakati baridi utawasadia. Bi Beatha anasema wao hawana vifungashio imara kwa ajili kufungia Siagi, wanaona wakipata vifungashio imara itaongeza thamani zaidi ya bidhaa zao. Bi Beatha anasema wanachangamoto ya usafiri kwa ajili ya kukusanya maziwa wakati wa kiangazi, kwa sababu ya uhaba wa upatikanaji wa maziwa hivyo wakipata usafiri wa uhakika utawasaidia kukusanya maziwa kwa urahisi.
Bi Beatha ameshukuru Halmashauri ya wilaya ya Karatu kwa kuwezesha kupata vifaa hivyo vinavyotumika katika shughuli zao za uuzaji wa maziwa. Lakini pia kwa kuendelea kuwapa mkopo ambao umewasaidia katika kupiga hatua zaidi katika shughuli zao za kuuza maziwa ya ng'ombe.
Karatu District Council
Sanduku la Posta: P.O Box 190
Simu: +255 272970648
Simu ya Mkononi: 0754773947
Barua Pepe: ded@karatudc.go.tz
Haki Miliki @ 2017 Halmashauri ya Wilaya ya Karatu.Haki zote zimehifadhiwa