Shirika la maendeleo la Japan ( JICA ) limefanya mafunzo elekezi kwa wataalamu wa kilimo wa wilaya juu ya namna ya kutekeleza mradi wa Tanshep. Mafunzo hayo yanafanyika katika ukumbi wa Halmashauri ya wilaya ya Karatu. Mafunzo yanahusisha wataalamu wa kilimo ngazi ya wilaya na kata, na yamelenga kuwajengea uelewa wa ndani namna kuutekeleza mradi, ambao unatarajia kuanza kufanya kazi katika wilaya ya Karatu kuanzia mwezi wa saba mwaka huu kwa muda wa miaka mitano.
Ndugu Greyson Makweta mkufunzi wa chuo cha kilimo cha mazao ya bustani Tengeru, amesema wizara ya kilimo kwa kushirikiana na shirika la maendeleo la Japan wamekubaliana kuanzisha mradi wa Tanshep. Ndugu Greyson amesema kauli mbiu ya mradi huo ni “anzia sokoni, malizia shambani, kwa kipato zaidi”. Mradi wa Tanshep umelenga kuwasaidia wakulima wadogo kwa kuanza na utafiti wa soko na kujua nani atamuuzia bidhaa yake. Kutokana na utafiti wa soko utakaofanywa na mkulima utamwezesha kujua ubora, pembejeo atakazotumia katika uzalishaji na mwisho wakulima watazalisha mazao yaliyo bora ambayo yatakidhi uhitaji wa soko. Ndugu Greyson amesema malengo ya mradi wa Tanshep ni kumfanya mkulima aongeze kipato, kwa kufuata taratibu mzuri wa kitaalamu ili kuweza kufikia malengo.
Ndugu Greyson amesema mradi Tanshep upo chini mpango wa ASTP 2 na mazao ya mboga mboga (horticulture) ni mazao ya kipaombele katika mradi. Kilimo cha mazao ya mboga mboga kina changamoto ya kupata soko la uhakika. Ndugu Greyson amesema mradi wa Tanshep umejikita katika kumuelekeza mkulima, namna ya kutafuta soko la mazao mwenyewe kabla ya kulima. Mradi ulibuniwa baada ya wakulima wengi kukosa masoko hasa kwenye mazao ya mboga mboga. Ndugu Greyson amesema katika kupata wilaya zitakazonufaika na mradi huo wataalamu wa kilimo wa wilaya waliandika madokezo yanayoeleza ubora wa wilaya zao katika kilimo cha mboga mboga. Baada ya kukaguliwa wilaya zilizoshinda katika mchakato huo ni wilaya ya Karatu na Arumeru kwa mkoa wa Arusha kwa Kilimanjaro ni wilaya ya Siha na Moshi vijijini na mkoa wa Tanga wilaya zilizoshinda ni wilaya ya Bumbuli na Lushoto.
Mafuzo elekezi kwa wataalamu wa kilimo katika ukumbi wa Halmashauri.
Ndugu Greyson anasema vigezo vilivyotumika kupata wilaya hizo ni, uzalishaji wa mazao ya mboga, lakini Halmashauri imetenga fedha kiasi gani kwa wakulima kusaidia kilimo cha mboga mboga (hortculture) pamoja na kuangalia miundo mbinu ya barabara ambavyo inawezesha kurahisisha bidhaa kufika sokoni kwa wakati. ndugu Greyson anasema waliangalia pia uwepo wa vikundi vya wakulima katika wilaya.
Mafunzo hayo ya siku mbili kwa wataalamu wa kilimo yanalenga kuwaongezea uelewa wa Tanshep ili nao wakatoe utaalamu huo kwa vikundi vya wakulima. Kwenye mradi huu wakulima watapata mafunzo kuhusu lishe na uelewa wa usawa wa kijinsia. Swala la uzalishaji shambani ni swala la familia na si swala la mtu mmoja. Ndugu Greyson amesema katika familia nyingi maamuzi yamekuwa ya mtu mmoja tu lakini sasa tunahitaji kuelimisha jamii ili swala la mamuzi liwe swala la familia. Ili familia iweze kufanikiwa kutoka kwenye kipato duni kuelekea katika maisha yaliyoboreka zaidi.
Ndugu Riziki Msite mtaalamu wa kilimo cha umwagiliaji Wilaya ya Karatu amesema semina ni kwa ajili ya kuelimisha wataalamu wa Halmashauri na siku ya pili ni kuwaelimisha maafisa kilimo wa kata na vikundi vya kilimo. Wilaya ya karatu kulikuwa na vikundi lakini vilikuwa havina uelewa wa kina, juu ya soko la mazao yao. Ndugu Msite amesema elimu waliyopata katika semina hiyo itasaidia kuwaelimisha wakulima namna ya kupata soko la mazao. Wilaya ya karatu ina vikundi nane vya wakulima; mbuga nyekundu imetoa vikundi vitatu, Dumbechand vikundi viwili, Mang’ola barazani kikundi kimoja, Maleckchand kikundi kimoja Laghangarer kikundi kimoja. Mradi huu ambao unajumuisha mikoa ya Arusha Kilimanjaro na Tanga kwa awamu ya kwanza utagharimu kiasi cha shilingi 1,754,380,000,000.
Karatu District Council
Sanduku la Posta: P.O Box 190
Simu: +255 272970648
Simu ya Mkononi: 0754773947
Barua Pepe: ded@karatudc.go.tz
Haki Miliki @ 2017 Halmashauri ya Wilaya ya Karatu.Haki zote zimehifadhiwa