Mkuu wa mkoa wa Arusha Mheshimiwa Mrisho Gambo jana amefanya ziara Wilayani Karatu. Katika kikao cha ndani kilichofanyika Ukumbi wa Mkuu wa Wilaya, alizungumza na watendaji mbalimbali wa Wilaya ya Karatu.
Mheshimiwa Mrisho Gambo amewaelekeza Wakuu wa Wilaya katika Mkoa wa Arusha, kupokea taarifa za miradi ya kila mwezi ili kuweza kujua mapungufu na changamoto zinazokabili miradi hiyo ili kuchukua hatua stahiki na miradi hiyo iweze kwenda haraka.
Mheshimiwa Mrisho Gambo amesema hajaridhishwa na makandarasi wa Maji Makina, ambaye alipewa miradi wa maji lakini miradi hiyo imeshindwa kufikia kiwango. Amesema Mkandarasi Makina alipewa mradi wa maji Kansay ambao alilipwa Million 444 kati ya million 467, lakini mkataba ulivunjwa baada ya kushindwa kufikia viwango vya ubora. Mkandarasi huyo akapewa mradi wa maji Burger ambao nao alilipwa million 359 kati ya million 413, mkataba ukavunjwa kwa sababu alishindwa kufikia viwango. Mkandarasi huyo akapewa mradi wa maji Matala akalipwa million 316 kati ya Million 375 mkataba ukavunjwa. Mheshimiwa Mrisho Gambo akamuelekeza Mkuu wa Wilaya Kuchukua hatua kali dhidi ya Mkandarasi huyo.
Mheshimiwa Mrisho Gambo alipokea taarifa ya mradi wa umeme vijijini REA phase three round one, Meneja wa Tanesco Karatu Ndugu Edward Mwakapuja alisema vijiji 9 vilikuwa kwenye mpango ambavyo vinajumuisha vitongoji 39. Alisema mpaka sasa Mhandisi amefanya kazi katika vijiji viwili tu ambavyo ni Kilimamoja na Kinihhe. Matarajio yetu mpaka sasa, kwenye mradi huu ni kwamba Mkandarasi angekuwa amefanya nusu ya kazi 50% lakini mpaka sasa Mkandarasi yupo chini ya 20%. Licha ya kuandikiwa barua ya onyo kutokana na utekelezaji mdogo wa mradi.
Mhandisi wa mradi huo NIPO GROUP L.T.D Engineer, Hussein Saidi alisema wanakutana na changamoto ya usambazaji duni kwa Wakala wa Usambazaji anayewaletea nguzo za umeme. Aliongeza kusema mahitaji ya nguzo kubwa za umeme ni nguzo 730 lakini wananguzo 257. Alisema mahitaji ya nguzo ndogo ni nguzo 1661 lakini nguzo walizo nazo ni 295. Engineer Hussein alisema wanauhitaji wa transfoma za umeme 50 lakini mpaka sasa wanatransfoma 21.
Mheshimiwa Mrisho Gambo amesema wananchi wanamatarajio makubwa ya kupata umeme katika makazi yao. Amesema sisi kama watendaji tunaomuwakilisha Mheshimiwa Rais lazima tutimize adhima ya kila sehemu kupata umeme ifikapo Mwaka 2021. Mheshimiwa Mrisho Gambo amewaonya watendaji wasio waadilifu wa Tanesco wanaowatoza wananchi zaidi ya kiwango kilichowekwa cha elfu 27000 ili kumuunganishia mwananchi na huduma ya umeme.
Karatu District Council
Sanduku la Posta: P.O Box 190
Simu: +255 272970648
Simu ya Mkononi: 0754773947
Barua Pepe: ded@karatudc.go.tz
Haki Miliki @ 2017 Halmashauri ya Wilaya ya Karatu.Haki zote zimehifadhiwa