NA TEGEMEO KASTUS
Kikao cha baraza la wafanyakazi kimepitisha bajeti ya matumizi ya fedha ya mwaka ujao wa fedha. kikao hicho kimekaa katika ukumbi wa Halmashauri na kimeongozwa na mwenyekiti wa baraza la wafanyakazi Halmashauri ya wilaya ya Karatu.
Ndugu Waziri Mourice Mwenyekiti wa baraza la wafanyakazi amesema haridhishwi na baadhi ya walimu ambao utendaji wa kazi wao ni mbovu. Amesema wilaya ya Karatu inawanafunzi wa kidato cha nne waliopata ufaulu wa daraja sifuri 986. Ndugu Mourice amesema hakuna sababu ya mwanafunzi kukaa miaka minne na kuishia kupata sifuri, kwa sababu mwanafunzi anayepata sifuri ina maana hanauwezo wa kupata daraja D mbili. Amesema kama Karatu sekondari wanafanya vizuri kwa wanafunzi wa kidato cha tano na sita, walimu wengine wanashindwaje kutumia mbinu hizo kwa wanafunzi wa kidato cha nne. Amesema Karatu sekondari wameongoza katika ufaulu wa kitaifa kwa somo la kilimo na amesema mwalimu huyo wa kilimo anapaswa kutambuliwa kama mwalimu hodari siku ya mei mosi.
Ndugu Mourice amesema amefanya ziara kata ya Mbulumbulu na kutembelea shule mbalimbali na amebaini hata orientation course kwa wanafunzi waliochaguliwa kuingia kidato cha kwanza hawakupata. Walimu wameanza kufundisha moja kwa moja, Maafisa elimu kata nao wameshindwa kusimamia ubora wa elimu katika maeneo yao. Orientation course ni muhimu ili kurahisishia wanafunzi wapate uwezo wa kuelewa na kupenda masomo. Sihivyo tu amesema kuna walimu wamekuwa wakijihusisha na mapenzi na wanafunzi wao, tuhuma hizo zimekidhiri na amesema atakabiliana na walimu wa aina hiyo. Kuna walimu Awet wanajihusisha na tuhuma hizo amezipokea na kuna walimu Glambo ambao nao wamehusishwa.
Ameshangazwa na watoto kuwa na nidhamu mbovu shuleni kiasi ambacho hawasimami hata kusalimia watu wazima pindi wanapotembelewa shuleni jambo linaloonesha usimamizi wahali chini wa nidhamu kwa wanafunzi shuleni. Amesema shule ya msingi kuna wanafunzi hawajui kusoma, amesema mwalimu mzuri anajitahidi na anahakikisha kila darasa hakuna mwanafunzi hata moja anakwenda darasa jingine bila kujua kusoma wala kuandika. Amesema Mwalimu mkuu unakaa ofisini kengele ya kipindi inagonga huendi kukagua kama walimu wameingia darasani. Amehoji kama mwalimu hujatimiza wajibu unapata wapi nguvu ya kudai haki, umefelisha wanafunzi unaanzaje kupata ufanyakazi bora. Imezuka tabia kwa walimu hasa wa kike wanaopata ujauzito kujipatia ruhusa kienyeji. Matukio kama hayo yametokea kwa walimu Glambo na baadhi ya shule nyingine, amesema kuna walimu wakuu wameshindwa kusimamia walimu wao. Amesema kwa hali kama hiyo watawavua vyeo walimu wakuu kwa kushindwa kusimamia utendaji kazi wa walimu shuleni.
Shule kama Bwawani inawalimu wa kutosha lakini bado zina wanafunzi hawajui kusoma na kuandika kuna shule ya Msingi Merera ambayo imekuwa ni moja ya shule zenye ufaulu duni. Ndugu Mourice amesema matokeo ni mabaya kiasi ambacho tume zinakuja kuchunguza chanzo cha ufaulu duni. Mbaya zaidi serikali imegharamika kuja na mtihani wa darasa la pili wa taifa kuja kupima wanafunzi.
Naye Katibu wa chama cha walimu mkoa wa Arusha ndugu Felix Mnyanyi amesema ualimu ni kazi ya kitume. Hakuna mwalimu anayeweza kutembea na wanafunzi asifahamike kwa sababu kuna fununu. Mahusiano ya mapenzi kati ya mwalimu na mwanafunzi huchangia kudidimiza ufaulu wa wanafunzi. Amesema kupanda madaraja sasa vigezo vitakavyoangaliwa ni uwezo wa kufaulisha na uwezo wa kufundisha. Amesema kweli daraja sifuri ndio linaloyumbisha matokeo ya ufaulu wa wanafunzi kwa mkoa wa Arusha. Ameomba wafanyakazi hodari wapatikane kutokana na utendaji wao wa kazi, amehimiza kutengwa kimakundi watendaji wabaya na watendaji wazuri . Amesema haitakuwa sawa kuwajumuisha wote kwa pamoja kwa sababu kuna kundi la walimu dhaifu kiutendaji na walimu bora kiutendaji.
Ndugu Felix amesema mafanikio ya shule yanatokana na uongozi, na pia mazingira ya shule husika, amesema kuna shule zinafanya vizuri. Shule zote Karatu zingekuwa zinafanya vibaya basi mkoa wa Arusha usingekuwa mkoa wa pili kwa ufaulu wa wanafunzi kitaifa.
Mwenyekeiti wa chama cha walimu wilaya ya Karatu Ndugu Vitalis Duke amesema kwamba kuna shida ya magari kwa idara za elimu. Maafisa elimu wanashindwa kufuatilia zaidi walimu katika vituo vyao vya kazi kutokana na ukosefu wa magari. Ufuatiliaji unasaidia kuinua utendaji wa kazi wa walimu na unaondoa mazoea katika kazi.
Ndugu Duke amesema hata Maafisa elimu kata nao bado hawajatumiwa vizuri, wameonekana kiutendaji kuachwa nyuma. Maafisa elimu kata wanapaswa kutumiwa katika kusimamia maendeleo ya elimu katika kata. Kuongeza uwajibikaji kwa mwalimu lakini pia kuongeza ushwawishi kwa wazazi kufuatilia maendeleo ya masomo ya watoto wao.
Karatu District Council
Sanduku la Posta: P.O Box 190
Simu: +255 272970648
Simu ya Mkononi: 0754773947
Barua Pepe: ded@karatudc.go.tz
Haki Miliki @ 2017 Halmashauri ya Wilaya ya Karatu.Haki zote zimehifadhiwa