Afisa elimu sekondari ametembelea shule za sekondari za serikali zinazofundisha kidato cha tano na sita kwa nyakati tofauti. Shule zilizotembelewa ni shule ya sekondari Karatu, Ganako na Florian, na amezungumza na wanafunzi wakidato cha tano wa shule hizo.
Bi, Kalista Maina alitembelea shule kogwe ya wavulana Karatu sekondari iliyopokea wanafunzi wapya 313 kati ya wanafunzi 345 waliopangwa. Wanafunzi 82 wamebadilishiwa shule na kujiunga na Karatu sekondari hivyo kufanya idadi kuwa 395. Shule ya sekondari wavulana Ganako ina wanafunzi 72 waliopangiwa kujiunga na kidato cha tano na wanafunzi 59 ndio walioripoti. Shule ya wasichana Florian ilipangiwa wanafunzi wa kidato cha tano 121 na wanafunzi walioripoti kwa ajili ya kuanza muhula wa masomo ni 108 na wanafunzi waliohamia kidato cha tano kutoka sehemu nyingine ni 10 hivyo kufanya idadi ya wanafunzi kufika 118.
Afisa elimu sekondari akiwa katika picha ya pamoja na walimu pamoja na wanafunzi wa kidato cha tano Karatu sekondari.
Bi, Maina amezungumza na wanafunzi hao wapya wa kidato cha tano, amewakumbusha wajibu wao kama wanafunzi. Amewaasa kusoma kwa bidii ili waweze kutimiza malengo, amewambia wanafunzi ili waweze kufaulu na kwenda kusoma ngazi ya chuo kikuu lazima wasome kwa bidii. Wazazi wanamatumaini makubwa sana, amewashauri kutunza na kuthamini muda, pamoja na kushirikiana kimasomo ili waweze kujengeana uwezo wa kitaaluma.
Naye Afisa elimu taaluma wilaya ndugu Robert Sijaona amewaambia wanafunzi hao wapya wa kidato cha tano, elimu ya kidato cha tano na sita ni tofauti na elimu ya kidato cha kwanza na nne. Ndugu Sijaona amewaambia vipo vitu vingi sana vya kusoma ndani ya muda mfupi amesema mambo mengine yasiyohusiana na shule tuachane nayo. Kupoteza mwanafunzi kwa sababu ya utovu wa nidhamu ni hasara kwa taifa na inaleta huzuni kwa wazazi. Fedha ya elimu pasipo na malipo inatolewa, walimu wanalipwa mishahara ili kuwafundisha, lazima muwe watii ili mfanye vizuri katika masomo yenu.
Ndugu Sijaona amesema tunataka wanafunzi wafaulu kwa kiwango cha daraja la kwanza na daraja la pili. Hata elimu ya ngazi ya juu udahili unapofanyika, wanafunzi wanaopewa mikopo na serikali ni wanafunzi waliofaulu vizuri kwa ngazi ya daraja la kwanza na lapili. Tunataka ufaulu wa daraja la tatu uwe ndio ufaulu wa chini kabisa na si vinginevyo. Ndugu Sijaona amewashauri wanafunzi kujihusisha na michezo baada ya muda wa masomo jioni, ili kuweka afya zao za mwili sawa.
Ndugu Sijaona akiwa florian amewahidi kuwaletea wanafunzi wa kidato cha tano na sita mwalimu wa kemia. Amesema shule ya Florian imekosa mwalimu wa kemia kwa muda mrefu, amewaahidi kuleta mwalimu ndani ya kipindi cha wiki mbili. Amewoamba wanafunzi kutoa ushirikiano wa kimasomo kwake pindi atakapofika na kuanza kuwafundisha.
Afisa elimu sekondari akiwa na wanafunzi wa kidato cha tano shule ya sekondari Florian.
Karatu District Council
Sanduku la Posta: P.O Box 190
Simu: +255 272970648
Simu ya Mkononi: 0754773947
Barua Pepe: ded@karatudc.go.tz
Haki Miliki @ 2017 Halmashauri ya Wilaya ya Karatu.Haki zote zimehifadhiwa