NA TEGEMEO KASTUS
Wananchi mnatakiwa kudumisha amani na utulivu, wakati shauri la msingi likiendelea kusikilizwa katika baraza la ardhi la wilaya ya karatu. Zuio la muda la kutoendeleza au kufanya shuguli zozote za maendeleo mpaka hapo shauri la msingi litakapoamuliwa lipo halali kisheria. Mnapaswa kusaidia kwa kutoa vielelezo vya msingi kwa mwana sheria ili viweze kuwakilishwa wakati wa usikilizaji wa shauri la msingi katika baraza la ardhi la wilaya.
Hayo yamesemwa na Mkuu wa wilaya ya Karatu Mh. Abbas Kayanda wakati akizungumza na wananchi wa kijiji cha Slahhamo Katika mgogoro wa kugombania eneo la ardhi kiasi cha hekari 32 na kanisa la KKKT Slahhamo kanda ya kaskazini, eneo ambalo wananchi wanadai lilitengwa na kijiji kwaajili ya kufanya shughuli za maendeleo ya kijiji. Mh. Kayanda amesema vurugu zilizofanywa na wananchi wakishinikiza kulitwaa eneo hilo sio sahihi, wananchi wanapaswa kusubiri mpaka shauri la madai ya ardhi litakapotolewa hukumu.
Wananchi wa kijiji cha Slahhamo wakiwa katika kikao
Mh, Kayanda amesema itakapotolewa hukumu na baraza la ardhi na nyumba, ikatokea hamjashinda taratibu zipo za kukatana rufaa ili shauri lisikilizwe upya katika mahakama kuu ya ardhi . Amesema Mwana sheria wa Halmashauri atasaidia kuchambua vielelezo katika shauri hilo ili kuona namna gani atasaidia kujenga utetezi na kulirudisha eneo lenye mgogoro kwenye Halmashauri ya kijiji cha Slahhamo. Shauri hilo la kesi lilianza tangu mwaka 2016 na litaendelea kusikilizwa mwezi wa tano mwaka huu.
Mh. Kayanda amesema kitendo kilichofanywa na baadhi ya watu kufanya uharibifu wa kuvunja madirisha ya kanisa la kinjili la Kilutheri Tanzania Slahhamo na kuweka vizuizi barabarani havivumiliki. Amesema wale wote watakaobainika kufanya uhalifu hatua za kisheria zitachukuliwa dhidi yao. Amesema serikali haiwezi kuingilia shauri ambalo limeshaingia kwenye vyombo vya kisheria. Ameomba wananchi kutofanya maamuzi wakati wakiwa wamegadhibika lazima mfuate utaratibu katika kudai haki.
wananchi wakiwa katika matukio tofauti wakati wa mkutano
Awali katika mkutano huo mwananchi Ndg. Harry Fabian amesema eneo ambalo linagombewa kati ya wananchi na kanisa la Kiluther Slohham yalikuwa maeneo ya wananachi. Amesema maeneo hayo yaliingia katika umiliki wa serikali ya kijiji baada ya wananchi waliokuwa wanamiliki maeneo hayo kufidiwa maeneo mengine ya mashamba na kijiji cha Slahhamo. Ndg Fabian amesema eneo hilo lilitwaliwa na kijiji kwa ajili ya kufanya shughuli za maendeleo kama kujenga zahanati na shule.
Ndg. Fabian amesema wanashangazwa kuona eneo hilo kuwa katika umiliki wa kanisa la Kiluther la Slahhamo, wakati vielelezo vyote vya umiliki wa eneo hilo wakiwa navyo serikali ya kijiji cha Slahhamo. Amesema kinachowaumiza zaidi ni zuio la muda lilowekwa na mahakama ya kutolitumia eneo hilo mpaka shauri la msingi limalizwe kusikilizwa. Amesema shauri hilo la kesi limechukua muda mrefu jambo ambalo linawavunja moyo.
Makamu mwenyekiti wa Halmashauri Mh. John Bayo amesema amewasikiliza vizuri malalamiko ya mgogoro wa wananchi na kanisa la Kiluther, amemuelekeza mwenyekiti wa kijiji kuleta vielelezo vya msingi, na wakutane katika Ofisi ya Mkurugenzi. Amewaomba wananchi wa kijiji cha Slahhamo kuwa watulivu na kuheshimu sheria, ili Mwana sheria aandae vielelezo vizuri vya kutetea shauri la msingi.
Afisa ardhi wa wilaya ya Karatu Ndg. Christopher Kitundu akisoma maombi ya zuio amesema sitisho la muda lililoombwa na kanisa la Kilutheri la kanda ya kaskazini Slahhamo mbele ya mahakama ni kuweka zuio kwa uongozi wa kijiji au muwakilishi kutofanya shughuli yoyote katika eneo lenye mvutano wa kijiji na kanisa. Amri hiyo ilitolewa na mahakama mwezi 1 tarehe 26 mwaka 2021.
Matukio Mbalimbali wakati wa mkutano
Karatu District Council
Sanduku la Posta: P.O Box 190
Simu: +255 272970648
Simu ya Mkononi: 0754773947
Barua Pepe: ded@karatudc.go.tz
Haki Miliki @ 2017 Halmashauri ya Wilaya ya Karatu.Haki zote zimehifadhiwa