Zoezi la maboresho ya daftari ya wapiga kura limefika katika siku yake ya mwisho. Siku ambayo watu wengi wamejitokeza kujiandikisha na kuboresha taarifa zao katika daftari la maboresho la wapiga kura. Halmashauri ya wilaya ya Karatu imesambaza vituo vingi vya kujiandikisha ili kuhakikisha kila mwenye sifa za kuboresha au kujiandikisha anapata nafasi hiyo.
Mkuu wa wilaya ya Karatu Mhe. Theresia Mahongo ni miongoni mwa viongozi waliojitokeza kuboresha taarifa zao katika daftari la wapiga kura. Amefanya maboresho katika kituo cha ofisi ya Katibu tarafa Karatu, amesifu utendaji kazi wa waandikishaji amesema zoezi linachukua muda mfupi na kupata kadi. Amesema nimeboresha taarifa zangu, katika daftari la wapiga kura kwa muda wa dakika mbili na kupata kadi yangu mpya ya kupiga kura.
Mkuu wa wilaya ya Karatu Mhe. Theresia Mahongo akiwa ameshika kadi yake mpya ya kupiga kura baada ya kufanya maboresho katika daftrari la wapiga kura.
Mhe. Theresia Mahongo amepongeza wananchi wa wilaya ya Karatu kwa mwitikio walioonesha, kwa kujitokeza kwenye zoezi uandikishaji wa daftari la maboresho ya kura. Amesema daftari hilo lililenga kuandikisha wapiga kura wapya, watu waliokuwa wamehama maeneo waliyokuwa wanaishi awali na watu ambao vitambulisho vyao vimevunjika au kuchakaa. Ametoa wito kwa wananchi kutunza kadi zao za kupiga kura vizuri ili waweze kuzitumia wakati wa uchaguzi. Uchaguzi mkuu wa Rais, wabunge na madiwani unatarajiwa kufanyika mwaka ujao mwezi wa kumi. Amesema kuboresha taarifa za wapiga kura ni moja ya hatua za kidemokrasia za kumwezesha mpiga kura kupiga na kuchagua viongozi anaowahitaji katika kipindi cha uchaguzi.
Zoezi la uandikishaji na maboresho ya daftari la wapiga kura limefanyika kwa muda wa siku saba wilayani Karatu na wilaya zote za mkoa wa Arusha. Muitikio umekuwa mkubwa kwa siku za mwisho wa zoezi hilo, ukilinganisha na siku za awali, jambo lililosababisha baadhi ya vituo kuwekwa mashine mbili ili kurahisisha zoezi la uandikishaji. Vituo ambavyo vimewekwa mashine mbili ni pamoja na kituo cha kujiandikisha cha bwawani shule ya msingi, kituo cha sokoni, kituo cha ofisi ya Tarafa. Vituo hivyo ni miongoni mwa vituo vilivyokuwa na msongamano mkubwa wa watu.
Naye ndugu Jonasi Iddi mkazi wa wilaya ya Karatu aliyejitokeza kuboresha taarifa zake, amesema zoezi limeenda vizuri kwa wilaya ya Karatu na limeleta hamasa kubwa kwa wananchi. Amesema watu wamejitokeza kwa sababu swala la uchaguzi ni swala nyeti. Watu wamejitokeza kwa sababu wanafahamu umuhimu wa kupiga kura. Amesema angetamani kila mmoja mwenye sifa za kujiandikisha au kuboresha taarifa zake awe amejitokeza kwa sababu inakupa nafasi ya kuchagua kiongozi unaye mtaka.
Karatu District Council
Sanduku la Posta: P.O Box 190
Simu: +255 272970648
Simu ya Mkononi: 0754773947
Barua Pepe: ded@karatudc.go.tz
Haki Miliki @ 2017 Halmashauri ya Wilaya ya Karatu.Haki zote zimehifadhiwa