Na Tegemeo Kastus
Hayati Rais. Dkt. John Pombe Magufuli ametujengea misingi imara ya uwajibikaji katika utawala bora, na amekuwa mtetezi wa wanyonge katika maeneo mbalimbali aliyopita. Tumeshuhudia namna watu wanavyolia juu ya kifo chake, tunapaswa kujifunza namna ya kutumikia wale tuliopewa dhamana ya kuwatumikia katika mambo yao.
Hayo yamesemwa na Mkuu wa wilaya ya karatu Mh. Abbas Kayanda wakati wa ibada ya kumuombea Hayati Rais, Dkt. John Pombe Magufuli iliyofanyika katika uwanja wa mazingira bora iliyojumuisha wananchi na watumishi. katika salamu zake Mh Kayanda amesema watu wameguswa na msiba wa hayati Rais Dkt John Pombe Magufuli, amefanya mambo mengi kwenye sekta ya afya sekta ya elimu, maji barabara usafiri na wameguswa na maendeleo yaliyofanywa.
Matukio katika picha wakati wanakwaya wakiimba katika ibada ya kumuombea hayati Rais. Dkt. John Pombe Magufuli
Amesema tumekuwa na bahati kubwa sana, ya miradi mingi ya maendeleo iliyoanzishwa na kwa imani tunaamini viongozi waliobakia wataifikisha miradi hii katika hatua iliyokuwa imedhamiriwa kufikiwa. Mh. Kayanda ameongeza kusema wanaamini hivyo kwa sababu mambo ya serikali yanaenda kwa taratibu zake. Akizungumzia swala la kuendelea kufanya ibada kwa ajili ya kumuombea kiongozi wetu, amesema ni vyema kutafakari sisi tuliobaki tumetanguliza nini kwa muumba wetu, kila mtu kwa imani yake. Amesema kifo ni safari ya wote na kila mtu ataondoka kwa wakati wake.
Katika salamu zake Mh. Kayanda amesema tumepata Rais mpya Mh. Mama Samia Suluhu Hassani amesema ni mama mchapakazi, mzalendo mtiifu muadilifu na mtetezi wa wanyonge. Mh Kayanda ameombwa wananchi kuwa na imani na kuendelea kumpa ushirikiano na kubwa ni kuendelea kumuombea kwa Mungu. Amesema kazi ya uongozi ni kazi inayohitaji kumtumaini mungu wakati wote, amesema tuendelee kuwapa moyo viongozi wetu na tuendelee kuwaombea kwa mwenyezi Mungu hakuna jambo litakaloshindikana.
Picha katika matukio Mbalimbali wakati wa ibada ya kumuombea hayati Rais. Dkt. John Pombe Magufuli Magufuli
Naye mwenyekiti wa chama cha mapinduzi wilaya ya Karatu, Ndg. Lusian Akonay amesema katika kipindi cha uongozi wake Hayati Rais. Dkt. John Pombe Magufuli alipenda kumshirikisha Mungu sana katika utendaji wake wa kazi. Ameongeza kusema amejenga umoja na mshikamano kwa watumishi wa umma na wananchi kwa ujumla, na amefanya mambo mengi sana katika muda wa uongozi wake.
Ndg. Akonay amesema sasa tumepata Rais mpya ambaye alikuwa Makamu wake wa Rais, anafahamu sana kazi zinazotakiwa kufanywa kwa sababu wote wameshiriki kunadi ilani ya chama cha mapinduzi yenye kurasa mia moja na tatu. Ndg. Akonay amesema Mh.Rais Mama Samia Suluhu atafanya vizuri zaidi, sisi kama wananchi tunapaswa kumuombea katika utendaji wa majukumu yake.
Mwenyekiti wa Halamashauri Mh. John Lusian amesema serikali ni juzi tuu imetoa kiasi cha billion moja kwa ajili ya ujenzi wa Hospitali ya wilaya ya Karatu na hospitali inatakiwa kukamilika mwishoni mwa mwezi wa sita. Mpango wa bajeti kwa mwaka ujao wa fedha, serikali imeahidi kutoa kiasi cha million 300 kwa ajili ya kuendeleza hospitali hiyo na kiasi kingine cha million 500 kwa ajili ya kununua vifaa vya hospitali. Mpango wa Mwaka ujao wa bajeti ya serikali imetenga fedha million 150 zitakazotumika kujenga zahanati zaidi serikali imetenga bajeti ya kujenga shule mpya ya sekondari wilayani Karatu iliyotengewa kiasi cha billion moja na million 200 bila kutegemea nguvu kazi ya mwananchi. Hizo zote ni ahadi alizotoa hayati Mh. Dkt. John Pombe Magufuli ameongeza kusema kwa sababu aliyeshika nafasi ya urais amesema kasi itaendelea ile ile tunatumaini kwamba haya yatafanyika ili kumuenzi hayati Dkt. John Pombe Magufuli.
Matukio mbalimbali wakati ibada ya kumuombea hayati Rais. Dkt. John Pombe Magufuli
Karatu District Council
Sanduku la Posta: P.O Box 190
Simu: +255 272970648
Simu ya Mkononi: 0754773947
Barua Pepe: ded@karatudc.go.tz
Haki Miliki @ 2017 Halmashauri ya Wilaya ya Karatu.Haki zote zimehifadhiwa