Mkuu wa Wilaya ya Karatu Mhe. Theresia Mahongo jana amefanya ziara katika kijiji cha Lositete. Katika ziara hiyo aliambatana na watendaji wa Wilaya, na alifanya mkutano wa hadhara na wananchi na kusikiliza changamoto zao mbalimbali.
Katika mkutano wake na wananchi wa kijiji cha Lositete Mhe. Theresia amehimiza wananchi kujenga vyoo bora. Kauli mbiu ya uhamasishaji wa ujenzi wa maliwato ni, NYUMBA NI CHOO. Amesema vyoo vingi ni vya kienyeji havijaezekwa vizuri, havina mlango na havijazibwa kwa juu. Tukijenga vyoo vizuri tutajiepusha na magonjwa ya mlipuko yanayoletwa kutokana na ukosefu wa vyoo na kutozingatia usafi wa afya zetu.
Mhe. Theresia amesema maradhi ni adui namba moja, amesema jinsi tunavyojenga nyumba bora tujenge na vyoo bora pia. Amesema wananchi tujali afya zetu, na tuzingatie yale tuliyoambiwa na wataalamu. Mhe. Theresia amegusia swala la ujenzi wa hospital ya wilaya ambayo kwa sasa msingi wa jengo la utawala na msingi wa jengo la wagonjwa wa nje umekamilika. Ameomba wananchi kujitolea kujenga hospitali ya wilaya, ili iweze kukamilika haraka.
Bibi Afya Sauda Leveri amesema choo bora kina ukuta wa matofali na lazima kiwe na mlango na uwe na kitasa ndani kwa sababu ya usiri. Choo cha asili kina shimo kwenda chini na sakafu ya udongo, ukuta wake unaweza kuwa wa miti uliokandikwa kwa udongo na mlango lakini pia huezekwa kwa paa au nyasi. Choo kilichoboreshwa kina bomba nje la kutolea hewa chafu, na inzi akiingia hawezi kutoka na hata akitoka anakufa. Choo cha maji kina sinki na kinatumia maji kuondoa uchafu, ( Smart latrine ) Choo chenye sinki kina kizibo kinachoziba tundu.
Awali katika taarifa yao iliyosomwa na ndugu Jakson Tango mwenyekiti wa kijiji cha Lositete amesema kitongoji cha Lengitima kina kaya zenye vyoo bora tano, na kaya zenye vyoo vya asili ni mia moja kumi na tatu. kitongoji cha Kituma kina kaya mbili zenye vyoo bora na kaya mia hamsini na tisa zina vyoo vya asili. Kitongoji cha Selela kina kaya moja yenye choo bora na kaya mia kumi na tisa zina vyoo vya asili.
Mwenyekiti ndugu Jakson amesema ofisi ya kijiji imefanya uhamasishaji kwa kutoa elimu na msako kwa kaya zisizo na choo. Amesema licha ya uhamasishaji huo bado kuna baadhi ya watu hawatumii maliwato. Kabla ya elimu ya uhamasishaji kutolewa kulikuwa na kaya mia na ishirini zilizokuwa hazina vyoo kabisa na kaya mia mbili sabini na moja zilikuwa na vyoo vya asili. Mwenyekiti ndugu jakson amesema kaya nane pekee ndizo zilikuwa na vyoo bora, amesema changamoto nyingine ni wananchi wengi kutoweka na kutumia vyombo vya kunawia mikono baada ya kutoka maliwatoni.
Bibi, Afya Sauda Leveri akieleza kwa vitendo jinsi ya kujenga choo bora.
Karatu District Council
Sanduku la Posta: P.O Box 190
Simu: +255 272970648
Simu ya Mkononi: 0754773947
Barua Pepe: ded@karatudc.go.tz
Haki Miliki @ 2017 Halmashauri ya Wilaya ya Karatu.Haki zote zimehifadhiwa