Na Tegemeo Kastus
Mkuu wa wilaya ya Karatu Mhe. Theresia Mahongo amewapa ndoo pamoja na sabuni za kunawa mikono maafisa Tarafa na maafisa watendaji kata wa kata zote za karatu. Zoezi hilo ni moja ya jitihada za kukabiliana na gonjwa la corona COVID-19.
Mhe. Mahongo amesema baada ya kuitisha kikao cha wadau wa afya mwezi wa tatu kujadili namna ya kupigana na janga la virusi vya corona; ikiwa ni pamoja na kuandika barua kwenye mashirika mbalimbali, Ofisi yake ilianza kupokea misaada kutoka kwa wadau. Mhe. Mahongo, amepongeza makanisa kwa kuchangia misaada mbalimbali, amesema kanisa la sabato, kanisa la Kkkt na kanisa Katoliki yametoa michango ya fedha. Mhe. Mahongo amesema vitu vingi alivyovikabidhiwa kwa maafisa Tarafa na maafisa Watendaji kata vimetoka kwa shirika la world vision.
Mhe. Mahongo amewaomba maafisa Tarafa na maafisa Watendaji kata kujikita katika kuelimisha watu juu ya ugonjwa wa virusi vya corona. Amesema kanuni za afya ni pamoja na kujali umbali wa mtu mmoja na mwingine, kuvaa barakoa na kunawa mikono kwa maji tiririka na sabauni. Amesema amepita kata ya Mang’ola akaona wananchi hawajali kuvaa barakoa kwa kisingizio ugonjwa haupo eneo lao. Ametoa maelekezo kwa Afisa Tarafa na watendaji kata kuweka mkazo katika elimu ya kuvaa barakoa.
Mhe. Mahongo amesema kwenye minada bado watu hawajahamasika kufuata kanuni za afya, ameomba maafisa hao kusimamia kikamilifu kwenye maeneo yao wakati wa shughuli za minada tahadhari zinazotolewa na wizara ya afya. Amesema kuna nchi ambazo hazijafanya lockdown lakini zinachukua tahadhari madhubuti zilizoainishwa na wataalam wa afya.
Katibu tawala wa wilaya ya Karatu Ndg. Abbas Kayanda amesema wananchi hupata huduma katika ofisi za watendaji kata na ofisi za tarafa katika maeneo yao. Amesema kwa kutambua mchango wa watendaji kata na maafisa Tarafa ni vyema watendaji hao wakajiweka katika mazingira salama katika utendaji wao wa kazi kwa kuchukua tahadhari juu ya janga la ugonjwa wa virusi vya corona.
Maafisa watendaji kata katika picha na mkuu wa wilaya Mhe. Theresia Mahongo
Karatu District Council
Sanduku la Posta: P.O Box 190
Simu: +255 272970648
Simu ya Mkononi: 0754773947
Barua Pepe: ded@karatudc.go.tz
Haki Miliki @ 2017 Halmashauri ya Wilaya ya Karatu.Haki zote zimehifadhiwa