Shirika la United Nations Development Programs (UNDP) kwa kushirikiana na wataalamu wa chuo kikuu cha SUA wamekabididhi mashine kumi za kutengenezea nishati mbadala ya kutumia masalia ya shambani. Makabidhiano yamefanyika mbele ya ofisi za Halmashauri ya wilaya ya Karatu.
Mgeni rasmi katika Makabidhiano hayo ya vifaa na mashine ni Mkuu wa wilaya ya karatu, ambaye aliwakilishwa na Ndugu Lameck Karanga Katibu Tarafa wa karatu. Ndugu Lameck amesema mashine hizo kumi ambazo zimegawiwa kwa vikundi kumi ni jitihada za kukabiliana na uharibifu wa mazingira. Ndugu Lameck ametoa salamu za shukrani na pongezi kutoka kwa Mkuu wa wilaya ya Karatu Mhe. Theresia Mahongo. Ndugu Lameck amesema tukio hilo ni tukio muhimu na rafiki kwa jamii yetu inayopakana na hifadhi ya Ngorongoro ambayo ni kivutio na kitega uchumi kwa taifa la Tanzania, amesema mradi huu wa kukabiliana na uharibifu wa mazingira utakuwa endelevu. Mradi huu utaifanya Karatu kuwa ya kijani kwa kuepukana na kukata miti hovyo. Ndugu Lameck amepongeza wataalamu kutoka SUA ambao wamesaidiana na shirika la UNDP amesema watendaji na wananchi wa Karatu ni waadilifu, watatunza mashine na matokeo mazuri ya matumizi ya nishati mbadala yataonekana.
NDUGU LAMECK KARANGA AKIKABIDHI MASHINE KWA WANAKIKUNDI KWA NIABA YA MKUU WA WILAYA YA KARATU
Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri Ndugu Godfrey Luguma, ameshukuru shirika la UNDP kwa msaaada wa vifaa hivyo kwa wanavikundi. Ameahidi kutumia wanavikundi kuongeza ufahamu wa kujifunza zaidi kuhusu nishati hiyo mbadala ambayo ni mkombozi kwa wananchi lakini pia kujenga fursa ya kiuchumi kwa kuzalisha nishati hiyo na kuiuza.
Naye Mhadhiri wa chuo kikuu cha sua Dkt. Nikson Peter Mkiramweni akisoma taarifa yake amesema mradi ulianza mwaka jana na kuzinduliwa rasmi 1/10/2018. Mradi uliandikwa na wanataaluma wa SUA, baada ya kukithiri kwa tatizo la kukata miti kwa ajili ya mkaa kwenye hifadhi ya Ngorongoro. Dkt, Nikson amesema waliamua kulipunguza hilo tatizo kwa kuleta nishati mbadala kwa kutumia masalia ya mbaazi, maganda ya karanga, vifuu vya nazi, maranda ya mbao lakini pia magunzi. Amesema lengo la mradi ni kuwajengea uwezo wanajamii na kutengeneza nishati mbadala na kuuza. Amesema wamefanya mafunzo kwenye vijiji ilikuwajengea uwezo wananchi katika vijiji na kuwapa mafunzo ya ujasirimali kwa vikundi. Amesema vikundi viliundwa kwa hiari, katika kujikita katika kuleta faida kwa wanakikundi, amesema wao kama wataalamu walifanya utafiti kuhusu soko la nishati hiyo na kugundua uhitaji wa soko kwa ajili matumizi ya nishati hiyo mbadala upo.
Dkt.Niksoni amesema mkaa huo mbadala unatumika kidogo kwa matumizi makubwa kulinganisha na mkaa wa kawaida kwa sababu unaungua kidogo kidogo. Amesema mkaa huo hauna moshi unaoumiza macho, amesema vifaa vilivyonunuliwa vimekabidhiwa kwa Halmashauri ya wilaya ili vikabidhiwe kwa wanavikundi.
Mmoja wa wanakikundi aliyekabidhiwa Mashine kutoka kikundi cha kilimamoja ndugu Faustini Bura amesema mashine hizo zitasaidia kuepusha uharibifuwa misitu kwa sababau mashine inatumia masalia ya mazao ili kutengeneza nishati ya mkaa. Tofauti na hapo awali uzalishaji wa mkaa kwa bishara na matumizi ya nyumbani ulitegemea kukata miti. Amesema mradi huo utawasaidia kiuchumi watafanya biashara ya mkaa mbadala ili kujitengenezea kipato.
MAPIPA YA KUCHOMEA NISHATI NA MASHINE KATIKATI VIKIWA VIMEPANGWA PAMOJA.
WANAKIKUNDI NA WATAALAM WAKISHIRIKIANA KUCHOMA KWA KUTUMIA PIPA LIKIWA MASALIA YA MBAAZI TAYARI KUTENGENEZA MKAA KAMA INAVYOONEKANA.
Karatu District Council
Sanduku la Posta: P.O Box 190
Simu: +255 272970648
Simu ya Mkononi: 0754773947
Barua Pepe: ded@karatudc.go.tz
Haki Miliki @ 2017 Halmashauri ya Wilaya ya Karatu.Haki zote zimehifadhiwa