Wanawake ni watu muhimu katika kukuza uchumi wa nchi na uchumi wa familia. Tunatakiwa tuendelee kupambana ili tuweze kutengeneza mazingira mazuri ya uchumi ili tuweze kuimarika kiuchumi na tuweze kusomesha watoto wetu na kushiriki katika ujasiriamali na vikundi vya vikoba.
Hayo yamesemwa na Bi, Faraja Msingwa Katibu tawala wa wilaya ya Karatu aliyemwakilisha Mkuu wa wilaya ya Karatu Katika kilele cha sherehe ya siku ya wanawake kilichofanyika katika uwanja wa Mazingira Bora Karatu. Kauli mbiu ya sherehe ya siku ya mwanamke ni mwanamke katika uongozi: chachu ya kufikia dunia yenye usawa.
Bi, Msigwa amehimiza wanawake kushiriki katika vikoba na saccos ikiwa ni pamoja na kujihusisha na ujasiriamali ili waweza kupata fursa ya mikopo inayotolewa na Halmashauri. Amesema idara ya maendeleo ya jamii inapaswa kuja na mkakati wa kutoa elimu ya Ujasiriamali kwa wanawake ili waweze kutambua fursa za uchumi zinazopatikana katika maeneo wanayoishi.
Bi Msigwa amesema serikali imeendelea kuthamini juhudi za maendeleo zinazofanywa na wanawake, hivi sasa serikali imeongeza jina la mwanamke katika hati kumiliki ardhi ili kujenga mazingira ya usawa katika haki ya kumiliki ardhi. Katika uongozi serikali bado imeendelea kujenga usawa wa kijinsia, kwa kuongeza nafasi za viongozi wanawake, ameongeza kusema wanawake wanapaswa kujitokeza kugombea na kushindana sera pindi fursa za uongozi zinapotangazwa.
Akizungumzia kuhusu mikopo Bi, Msigwa amesema lazima kuwe na nidhamu ya kukopa mikopo kwenye vikundi, amesema wanawake wamekuwa na tabia ambayo si nzuri ya watu kuchukua fedha za mikopo na kufanya shughuli ambazo hazisaidii kumjengea uwezo mkopaji kurudisha fedha kwa wakati. Amesema ni vyema wanawake watambue umuhimu wakujishughulisha katika shughuli za maendeleo ili mikopo iweze kusaidia kuimarisha shughuli za uzalishaji.
Katibu tawala wa wilaya ya Karatu Bi, Faraja Msigwa (katikati) pamoja Na Mwenyekiti wa Halmashauri Mh. Lucian wakiwa wameshikilia check tayari kwa kukabidhi vikundi 96 vya wakinamama vijana na walemavu.
Awali katika risala yao wanawake wa Halmashauri ya wilaya ya Karatu iliyosomwa na Bi, Honoratha Sulle amesema vitendo vya ukatili wa kijinsia vinawaelemea zaidi wanawake na watoto. Amesema jamii, vyama vya siasa vinapaswa kuwa na mtizamo chanya juu ya maendeleo ya wanawake, ikiwa ni pamoja na kurekebisha mila na desturi zinazowabagua wanawake.
Amesema jamii inapaswa ihamasishe kwa ujumla juu ya umuhimu wa utekelezaji shughuli mbalimbali za serikali kwa malengo ya kudumisha amani na upendo. Amesema hiyo itasaidia kujenga mshikamano kwa wanawake wote ambao utawekewa msisitizo katika kauli mbiu za siku ya mwanamke ili kujenga umoja. Amesema utaratibu wa kukemea mfumo dume uliopo imesaidia kupunguza adha wanazokumbana nazo wanawake katika maisha ya kila siku.
Bi, Sulle amesema lazima wanawake wahamasishwe kupeleka vijana wao wa kike shule, huku wakiendelea kupewa elimu ya jinsia na maendeleo kwa malengo ya kung’amua fursa za uchumi walizonazo katika mazingira yanayowazunguka ikiwa ni pamoja na kuwapa ujuzi.
Matukio mbalimbali wakati wa maadhimisho ya siku ya wanawake katika uwanja wa mazingira Bora
Karatu District Council
Sanduku la Posta: P.O Box 190
Simu: +255 272970648
Simu ya Mkononi: 0754773947
Barua Pepe: ded@karatudc.go.tz
Haki Miliki @ 2017 Halmashauri ya Wilaya ya Karatu.Haki zote zimehifadhiwa