Kamati ya siasa ya chama cha mapinduzi imefanya ziara katika Tarafa ya Eyasi na kutembelea miradi mbalimbalimbali ya maendedeleo. Ziara hiyo iliyoingia siku ya pili imetembelea miradi ya elimu na afya na kutoa maelekezo mbalimbali kwa watendaji wa Halmashauri.
Mwenyekiti wa chama cha mapinduzi ndugu Lucian Akonay amesema ujenzi wa jengo la nyumba ya walimu (two in one) Kisimagenda uko chini ya kiwango. Amesema jengo limewepewa million 20 na zimetumika wakati mradi ukiwa bado chini ya kiwango. Hakuna ujenzi wa aina hiyo kama kulikuwa na hitilafu awali kwenye msingi wa jengo hatua zilipaswa kuchukuliwa awali badala ya kuendelea na ujenzi mpaka kufikia hatua ya upauzi.
Muonekano wa jengo la nyumba ya walimu Kisimagenda kwa upande wa juu
Mwenyekiti wa chama ndugu Lucian Akonay ametoa maelekezo kwa watendaji wa serikali kushughulikia wahusika wote katika ujenzi wa nyumba hiyo ambayo imebaki kama gofu. Amesema kuna uzembe mkubwa umefanywa katika ujenzi wa jengo, lazima tuwajibishane kwa namna ambayo itasaidia ujenzi wa nyumba kufanyika. Pamoja na kutambua watu waliohusika na ubadhilifu ni vyema ikapatikana njia ya kufanya mradi wa ujenzi wa nyumba ya walimu shule ya Kisimangeda unafanyiwa kazi ili kupunguza tatizo la uhaba wa nyumba za walimu. shule ya Kisimangeda haina nyumba hata moja ya mwalimu katika eneo la shule jambo linalochangia pia kudidimiza maendeleo ya taaluma katika shule hiyo.
Mkuu wa wilaya ya Karatu Mhe. Theresia Mahongo ambaye alikuwa katika ziara hiyo amesema amesikitishwa na ujenzi wa chini ya kiwango wa jengo hilo la walimu. amesema jengo hilo halifai kuishi mtu, kwa sababu hata matofali yaliyojengwa kwenye jengo hilo yanapuputika. Ameongeza kusema watendaji wa shughuli za serikali wafike mahali waone aibu kwa matumizi mabaya ya fedha za umma. Mkuu wa wilaya Mhe. Theresia ametoa maelekezo ya kumsimamisha mtendaji wa kijiji ndugu Amani Mehad na kuwekwa ndani wakati watendaji wa Halmashauri waliohusika ambao wengi wao wamehamishwa hatua za kinidhamu zikichukuliwa dhidi yao.
Mkurugenzi mtendaji wa Halmashauri ndugu Waziri Mourice amesema ni kweli kuna ubadhilifu umetokea. Amesema awali tatizo hilo lilionekana na walimuelekeza mwandisi wa Halmashauri kulikagua jengo hilo na kutoa mapendekezo baada ya kusimamisha ujenzi. Amesema baada ya ukaguzi wa mwandisi alipendekeza jengo hilo kuwekewa nguzo kila pembe ya ukuta ili kuongeza uimara wa jengo. Amesema maelekezo hayakufanyiwa kazi na wameendelea na hatua za ujenzi hadi kufikia hatua ya upauzi. Ndugu waziri amesema hata upauzi unadosari kwa sababu wamepauwa nyumba kwa bati za geji 30. Mafundi waliojenga jengo wanaonekana hawana ustadi wa ujenzi, ukuta umepinda na kwa sababu wameharakisha jengo mpaka kufikia hatua za upauzi inaonesha dhahiri kuna kitu kinafichwa.
Muonekano wa jengo zima la nyumba ya walimu Kisimagenda.
Awali katika taarifa yake Mtendaji wa kijiji ndugu Amani Mehad amesema ujenzi wa jengo hilo ulianza 20/9/2016 (kwa nguvu za wananchi) mapato ya ndani ya kijiji. Ndugu Amani amesema wakati ujenzi umefika kwenye lenta chini ya madirisha kwa gharama za wananchi kiasi cha million 4 na laki 5 zilitumika. Halmashauri ilitoa million 20 kuendeleza ujenzi wa jengo hadi kufikia hatua ya kupauwa jengo. Amesema changamoto ya ujenzi wa jengo hilo ni kwamba ujenzi ulisimamishwa na mwandisi wa Halmashauri kwa sababu matofali yalikuwa chini ya kiwango na changamoto hiyo ilishughulikiwa.
Naye mwalimu mkuu wa shule ya msingi Kisimagenda Victoria Wilson Mosha ameomba serikali kujenga nyumba hata moja ili iwarahishie katika shughuli zao za kitaaluma. Walimu wote wanakaa nje ya eneo la shule na wanalazimika kutembea umbali wa km 4 kufika shuleni. Amesema hata utunzaji wa mazingira ya shule umekuwa na changamoto kwa sababu eneo hilo limepandwa miti lakini kwa sababu ya kukosa usimamizi wanyama wa wanaofugwa nyumbani wanaharibu miti hiyo.
Karatu District Council
Sanduku la Posta: P.O Box 190
Simu: +255 272970648
Simu ya Mkononi: 0754773947
Barua Pepe: ded@karatudc.go.tz
Haki Miliki @ 2017 Halmashauri ya Wilaya ya Karatu.Haki zote zimehifadhiwa