NA TEGEMEO KASTUS
Ukipewa dhamana ya uongozi unatakiwa uwe mfano kwenye jamii kwa kuishi kwa maadili ya uongozi ili uweze kuongoza wananchi vyema. Uongozi sio kujiamulia mambo kadri unavyotaka wewe mwenyewe, kutumia madaraka vibaya ni makosa kisheria. Tabia ya matumizi mabaya ya madaraka imezidi kushamiri sana kwa watendaji wa vijiiji.
Hayo yamesemwa na Mkuu wa wilaya ya Karatu Mh. Abbas Kayanda wakati alipofanya kikao cha ndani na viongozi na watendaji katika kata ya oldean. Amesema kumekuwa na tabia ya watendaji kukusanya fedha na kukaa na fedha mbichi bila kupeleka fedha benki. Fedha yoyote au mchango lazima uwekwe katika akaunti ya kijiji benki na kutoa kwa muhtasari wa vikao halali utakaoidhinishwa na Halmashauri ya kijiji. Akizungumzia tabia ya uzwaji wa viwanja kiholela bila kufuata utaratibu Mh. Kayanda amekemea tabia za viongozi wa vitongoji kujihusisha katika uzaji wa ardhi na badala yake ameelekeza wananchi wenye uhitaji wa viwanja kuenda kwa mwenyekiti wa kijiji ili kupata utaratibu wa kununua viwanja.
Akizungumzia kuhusu adha ya maji katika kata ya Oldean Mh. Kayanda amesema haridhishwi na utendaji wa kazi wa viongozi wa jumuiya ya watumia maji Gewasu. Mh. Kayanda ameelekeza meneja wa Ruwasa wailaya Mhandisi Kilangai kufuatilia na kujiridhisha juu ya matumizi ya fedha ya jumuiya hiyo ya watumia maji Oldean kabla ya kumaliza muda wao wa uongozi mapema mwezi wa tisa mwaka huu. Amesema kuna upatikanaji wa maji usioridhisha katika kata ya Oldean ametoa wito kwa viongozi wa jumuiya ya watumia maji kujipanaga na kuhakikisha maji yanapatikana muda wote. Dhamana ya uongozi ni kutafutia ufumbuzi matatizo ya wananchi, kama kuna wateja wa maji ambao hawana bili za maji wapewe ili kuwe na usimamizi wa maji mzuri ambao hautatoa mianya ya rushwa.
Mh. Abbas Kayanda akizungumza na viongozi na watendaji wa serikali katika kikao cha ndani Oldean sekondari
Ameongeza licha ya chanagamoto hizo bado watu walioteuliwa kufanya kazi ya kufungua maji hawafanyi kazi hiyo kwa ufanisi na badala yake wamekuwa wanafungua maji kwa namna wanavyotaka wao. Mh. Kayanda amekemea tabia hiyo amesema si tabia njema kwa sababu inaleta mazingira ya rushwa. Amesema kuna uhitaji wa kuweka bomba kubwa la maji ili kuongeza nguvu ya maji kutoka kwenye mabomba lazima jumuiya ya maji iwe na uwezo wa kuiendesha ili kufikia malengo hayo.
Mh. Abbas Kayanda (kushoto) akizungumza na Mh. Peter Mmasi (katikati) alipoembelea jengo la mortuary katik kituo cha afya Oldean
Akizungumzia kuhusu unywaji wa gongo na kamari Mh. Kayanda amekemea tabia ya wananchi kujikita katika ulevi na kamari katika kata ya Oldean. Amesema jambo hilo imekuwa likififisha nguvu kazi ya uzalishaji. Amesema lazima watendaji wasimamie sheria bila kuonea mtu na kuhakikisha vitendo vya uchezaji wa kamari na unywaji wa gongo vinaisha na watu wanajikita katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo. Amesema vijana wanapaswa kujiunga katika vikundi ili kupata mikopo ya Halmashauri inayotolewa na serikali bila riba badala ya kujikita kwenye uchezaji wa kamari.
Mh. Abbas kayanda alipotembelea kivuko cha Oldean ng'ambo na kivuko cha posta katika ziara ya kukagua miundo mbinu ya barabara kata ya Odean
Katika hatua nyingine Mh. Kayanda ametembelea na kujionea vivuko viwili ambavyo ni kivuko cha posta, na kivuko Oldean ng’ambo ambavyo wanafunzi hupata adha ya kuvuka wakati mvua zinaponyesha. Ameelekeza viongozi wa kijiji kukaa na wataalmu wa Tarura kufanya usanifu wa vivuko hivyo ili kujua gharama halisi za utengenezaji ili kusaidia kuweka katika bajeti ya serikali ya kijiji baadae taaarifa hiyo iingizwe kwenye bajeti ya Tarura mwaka ujao wa fedha.
Mh. Kayanda amehimiza watendaji kutenga siku maalumu kwa ajili ya kusikiliza na kutatua kero za wannchi katika maeneo yao ya utendaji. Amesema kusikiliza kero za wananchi kunasaidia kuanza kufanya ufutiliaji mapema na kutafutia ufumbuzi wa matatizo ya wananchi.Amehimiza viongozi kuwa mfano wa kuvaa barakoa na kuhimiza wananchi kuvaa barakoa na kunawa kwa maji tiririka na vitakasa mikono ikiwa ni pamoja na kuepuka misongamano na kufuata muongozo wa serikali ulitolewa kupitia wizara ya afya juu ya namna ya kuchukua tahadhari dhidi ya maradhi ya ukovi.
Wakati huo huo Mh. Kayanda ametembelea shule ya msingi Oldean kujionea miundo mbinu ya elimu. Katika ziara hiyo Mh. Kayanda ameelekeza taasisi ya kuzuia na kupambana na rushwa kufanya ukaguzi katika shule hiyo ili kujiridhisha na mapato na matumizi ya shule ya msingi Oldean. Katika hatu nyingine Mh. Kayanda ametembelea kituo cha afya Oldean na kukagua urekebishaji wa jengo la kufulia jengo la wodi na jengo la kuhifadhi maiti. Mh. Kayanda ameonesha kutoridhishwa na matumizi ya fedha za uakarabati wa miundo mbinu ya afya katika kituo hicho na hivyo kuagiza taasisi ya kuzuia na kupambana na rushwa kufanya ukaguzi juu ya namna matumizi ya fedha ukarabati wa jengo la kufulia na ukarabati wa jengo la wodi ili kujiridhisha kama fedha zilizotolewa kama zinaendana na thamani ya ukarabati uliofanyika.
Mh. Kayanda ametoa rai kwa watendaji wa serikali katika miradi ya afya na elimu kuhakikisha fedha zinazotolewa na serikali kwa ajili ya ujenzi na uboreshaji wa miundo mbinu ya afya na elimu utumiaji wake kuwa unahusisha kikamilifu kamati ya ujenzi ya eneo husika. Amesema kumekuwa na shida ya watendaji wa serikali kufanya shughuli za ujenzi bila kuunda kamati ya ujenzi jambo linaloweka mashaka juu ya usimamizi wa miradi ya ujenzi kulingana na thamani ya fedha iliyotolewa na serikali.
Karatu District Council
Sanduku la Posta: P.O Box 190
Simu: +255 272970648
Simu ya Mkononi: 0754773947
Barua Pepe: ded@karatudc.go.tz
Haki Miliki @ 2017 Halmashauri ya Wilaya ya Karatu.Haki zote zimehifadhiwa