NA TEGEMEO KASTUS
Mazingira mazuri ya kufundisha yanapaswa kutengenezwa na kuwekwa vizuri ili mwanafunzi aweze kusoma katika mazingira rafiki. Ufaulu wa shule za msingi unapaswa kuanzia alama tisini na kuendelea, ni vyema kuongeza uwajibikaji ili kuinua kiwango cha elimu. Walimu wakae karibu na maeneo yao ya vituo vya kazi ili kuongeza ufuatiliaji wa taaluma kwa wanafunzi.
Hayo yamesemwa na Mkuu wa wilaya ya Karatu Mh. Abbas Kayanda alipotembelea shule ya msingi Marar kukagua miundo mbinu ya elimu. Shule ya Marar ambayo ina wanafunzi miamoja na themanini na sita na ufaulu wake wa mitihani ya taifa ni alama hamsini. Mh. Kayanda amebaini usimamizi dhaifu wa kiutawala kwa mkuu wa shule, jambo linalochangiwa na mkuu huyo wa shule kuishi mbali na kituo chake cha kazi. Uongozi wa shule kushindwa kuweka mazingira ya shule katika hali ya usafi ili wanafunzi kusoma katika mazingira mazuri.
Mh. Abbas kayanda akikagua miundo mbinu katika shule ya msingi Marar
Mh. Kayanda amesema ni vyema walimu wakajiepusha na vitendo vya utoro mahali pakazi jambo ambalo linachangia kuzorotesha elimu. Mwanafunzi ili ajifunze anahitaji ufuatiliaji wa karibu, ameelekeza waratibu wa elimu kata, kuwa na utaratibu wa kutembelea shule zilizokaribu na maeneo yao kujionea na kujiridhisha na mazingira ya ufundishaji na ufundishwaji ili kuboresha kiwango cha ufaulu wa elimu.
Maelekezo hayo yameenda kwa viongozi wengine kama maafisa tarafa watendaji kata na watendaji wa wakijiji lengo likiwa ni kujenga utaratibu wa kutembelea taasisi zinazowazunguka na kuzitambua changamoto zao. Kuzitafutia ufumbuzi na kuwasilisha kero zilizo nje ya uwezo katika ngazi za juu za maamuzi. Mh. Kayanda amesema hiyo ndio namna nzuri ya kuongeza ufanisi wa kazi kuanzia chini mpaka ngazi za juu.
Katika ziara hiyo Mh. Kayanda ametembelea na kujionea ujenzi wa matundu vyoo katika shule ya sekondari Kilimatembo na Diego. Amesema lazima ujenzi wa majengo hayo ya vyoo uendane na thamani ya fedha inayotolewa. Shule ya sekondari kilimatembo ujenzi wa matundu kumi ya vyoo, matundu matano kwa ajili ya vyoo vya wavulana na matundu matano mengine ya vyoo kwa ajili ya wasichana. Mh. Kayanda ametoa angalizo kwa watendaji kujiepusha na vitendo vya ubadhilifu wakati wa ujenzi ili thamani ya fedha inayotolewa iendane na thamani ya ujenzi.
Mh. Kayanda ameoneshwa kutoridhishwa na gharama kubwa za ujenzi wa vyoo katika shule ya sekondari ya Diego. Amesema haiwezekani kujengwa matundu kumi ya choo kwa kiasi cha million ishirini na nne mpaka kukamilika. Amesema zipo taasisi ambazo zimefanya ujenzi wa vyoo kwa idadi hiyo hiyo ya matundu kumi ya choo lakini kwa gharama za chini. Ameelekeza kamati ya ujenzi ya shule ya sekondari Diego kufanya upembuzi upya wa gharama za ujenzi wa maliwato ili kujiridhisha wakati ujenzi wa vyoo ukiwa unaendelea. Lengo likiwa ni kujiepusha na matumizi mabaya ya fedha.
Mh.Abbas Kayanda akiwa katika eneo la ujenzi wa vyoo shule ya sekondari Diego
Karatu District Council
Sanduku la Posta: P.O Box 190
Simu: +255 272970648
Simu ya Mkononi: 0754773947
Barua Pepe: ded@karatudc.go.tz
Haki Miliki @ 2017 Halmashauri ya Wilaya ya Karatu.Haki zote zimehifadhiwa