Na Tegemeo Kastus
Kamati ya ujenzi wa zahanati ya Mang’ola juu imetakiwa kuwasilisha nyaraka na vielelezo vyote vinavyohusiana na ujenzi wa nyumba ya wauguzi two in one. Hatua hiyo inakuja baada ya gharama za ujenzi zahanati hiyo kutoendana na thamani ya ujenzi wa jengo hilo. Hatua hizo zinakuja ili kudhibiti tabia ya ufujaji wa fedha kwa kamati za ujenzi zinazopewa dhamana ya kusimamia miradi ya maendeleo katika kuimarisha upatikanaji wa huduma za jamii.
Mh. Kayanda akikagua na ujenzi wa miundo mbinu ya ujenzi wa nyumba ya wauguzi Mang'ola juu
Hayo yamejiri katika ziara ya Mkuu wa wilaya ya Karatu Mh. Abbas kayanda alipotembelea taasisi za serikali zilizopo katika kijiji cha Mang’ola juu. Mh. Kayanda ameonesha kutoridhishwa na hatua za ujenzi wa nyumba hiyo baada ya kubaini mapungufu katika ujenzi ikiwemo, vifaa vya ujenzi vienye ubora duni. Zahanati hiyo ni moja zahanati tatu zilizopewa kiasi cha shilingi million 50 kwa ajili ya umaliziaji ujenzi wa miundo mbinu ya afya katika zahanati. Ameelekeza uchunguzi wa kina kufanyika katika jengo hilo ili kujiridhisha na kiasi cha fedha kilichotumika. Ametoa rai kwa watendaji wa kijiji kusimamia vizuri ujenzi wa miradi ya maendeleo katika maeneo yao ya utawala.
Mh. Kayanda akikagua ujenzi wa jengo la wauguzi, katika zahanati ya Mang'ola juu.
Katika zaira hiyo Mh. Kayanda ametembelea shule ya msingi Mang’ola juu kujioenea mazingira ya ufundishaji na ufundishwaji. Amehimiza wanafunzi kusoma kwa bidii na kuepuka tabia za utoro, na kuelekeza watendaji kuhakikisha mwanafunzi hawakosi shule kwa sababu ya mzazi kushindwa kuchangia amesema watoto ndio hazina ya kesho hivyo wanapaswa kusoma katika mazingira mazuri.
Mh. Kayanda ameelekeza kuwepo kwa vyuma vya kuondolea matope mbele ya milangoya madarasa ili kuweka usafi wa madarasa katika mazingira mazuri. Katika hatua nyingine Mh. Kayanda ameelekeza uongozi wa serikali ya kijiji kupitia mkutano mkuu kuja na mpango wa ujenzi wa darasa moja katika shule ya Mango’ola juu ili kuongeza vyumba vya madarasa. Wakati huo huo ameelekeza darasa la awali ambalo limekuwa limebaki bila kutumika kufanyiwa ukarabati ili wanafunzi waanze kulitumia mapema mwanzoni mwa wiki ijayo.
Mh. Kayanda akizungumza na wanafunzi wa shule ya msingi Mang'ola juu
Akizungumza na viongozi wa Halmashauri ya kijiji Mh. Kayanda amesema serikali imetoa kiasi cha shilingi billion moja kwa ajili ya ufunguzi wa barabara sita mojawapo mwa barabara itakayofunguliwa ni kutoka kibaoni, mang’ola juu kuelekea makoromba. Ameongeza kusema mradi wa Rea wa awamu ya tatu mzunguko wa pili uliohusisha kijiji cha Mang’ola juu, ambao ulisimama umepewa mkandarasi mwingine kampuni tanzu ya Tanesco anayeshughulikia miradi yote ya viporo ya awamu hiyo. Amesema mradi huo utatekelezwa na kijiji cha Mang’ola kitapata umeme; Mh. Kayanda ameendelea kuhimiza wenyeviti wa vijiji kusoma mapato na matumizi kwa wakati, kutosoma mapato na matumizi ni kuonea wananchi, ambao wanauhitaji kufahamu tarifa za fedha kila robo ya mwaka. Amesema hali hiyo ndio inafanya watendaji kushindwa kukaa na wananchi na kujadili ujenzi wa miradi ya maendeleo.
Mh. Kayanda amesema watendaji wa vijiji wanapaswa kubadilika kwa kutenga siku za kukaa ofisini na siku za kutembelea miradi na taasisi zilizo katika maeneo ya utawala wa Halmashauri ya kijiji ili kujua changamoto zao na kuzitatua. Amesema ni jukumu la watendaji wakijiji kusimamia sheria katika kukabiliana na utoro wa wanafunzi, amesema kupitia kamati za huduma ya jamii ni jukumu lao kufuatilia wanafunzi watoro kwa kuwachukulia hatua za kisheria kwa wazazi wao. Amesema watendaji wanatakiwa kuhamasisha wananchi katika ujenzi wa vyoo bora na kukabiliana na watu wanaojihusisha na uchezaji wa pooltable muda wa asubuhi.
Mh. Kayanda katika matukio tofauti wakati akikagua miundo mbinu ya elimu katika shule ya msingi Mang'ola juu.
Mh. Kayanda amesema watendaji wa kijiji waendelee kuelimisha wananchi kujitokeza kwa hiari kupata chanjo ya ugonjwa wa ukovi, ikiwa ni pamoja na kuelimisha jamii juu ya namna kuchukua tahadhari kwa wananchi kwa kufuata miongozo ya wizara ya afya kama kuvaa barakoa na kunawa mikono mara kwa mara na kwa maji tiririka. Ameendelea kuhimiza kutumia vitakasa mikono na kuepeuka misongamano ya watu kwa kukaa umbali wa mita moja ili kundelea kujikinga na ugonjwa wa ukovi-19.
Karatu District Council
Sanduku la Posta: P.O Box 190
Simu: +255 272970648
Simu ya Mkononi: 0754773947
Barua Pepe: ded@karatudc.go.tz
Haki Miliki @ 2017 Halmashauri ya Wilaya ya Karatu.Haki zote zimehifadhiwa