Waziri wa Maji Profesa Makame Mbarawa amefanya ziara ya siku moja wilaya ya karatu. Amekagaua miradi ya maji katika tarafa ya Karatu mjini na tarafa ya Endabash na kupokea taarifa ya miradi ya maji ya wilaya.
Waziri wa maji ametoa kiasi cha Million 300 kwa kuanzia kwa ajili ya undelezaji wa miradi ya maji wilayani Karatu. Miradi ya maji ambayo itaanza kufanyiwa kazi kutokana na fedha hizo ni mradi wa maji Ayalabe kata ya Ganako; mradi wa maji bwawani kata ya Karatu, mradi wa maji Kansay kata ya Kansay na Mradi wa Maji Buger kata ya Burger. Amesema watatumia force account katika utekelazaji wa miradi hiyo na vifaa vitanunuliwa kwa pamoja ili kupunguza gharama za manunuzi. Mhe. Waziri wa Maji Profesa Mbarawa amesema watajikita katika ununuzi wa mabomba, watajikita katika ununuzi wa pampu za maji na kuanza kutoa fedha kidogo kwa ajili ya ujenzi wa matanki ya maji mawili.
Mhe. Waziri wa Maji Profesa Mbarawa ametembelea mradi wa kwa Tom ulipo karatu Mjini. Katika mradi huo Mhe. Waziri Profesa Mbarawa amesema upatikanaji wa maji upo chini sana wilayani karatu. Gharama za mradi wa maji kwa Tom ni takribani million 500 na gharama zilizobakia ili kukamilisha mradi ni million 209. Mhe. Waziri ameahidi kutoa fedha za mradi huo zilizobaki mwezi huu, ili kuhakikisha mradi umemalizika kwa 100% kwa sasa mradi ujenzi wake umefika 75%. Amesema mradi huo ukimalizika upatikanaji wa maji katika mji wa Karatu utafikia 52%.
Katika kikao cha ndani Mhe. Waziri wa Maji na Umwagiliaji Profesa Mbarawa amesema miradi ya maji kwa kipindi kirefu haikufanywa kwa viwango vinavyostahili. Amesema sisi wote hatukuwafanyia wananchi haki, ndio maana tumeanzisha RUWASA na kuhakikisha miradi yote ya maji inatekelezwa. Profesa Mbarawa amesema jambo la pili ni kuhakikisha wakandarasi wa hovyo tunaachana nao na kazi zinafanywa na wataalamu wa RUWASA. Profesa Mbarawa amesema mpaka sasa hakuna kibali kilichotolewa kwa mkandarasi yeyote wizarani. Hatua za kisheria zinaendelea kuchukuliwa dhidi ya wakandarasi wazembe, Profesa Mbarawa amesema jambo la kwanza kwa sasa kwa watanzania ni kuhakikisha tunaleta maji safi na salama.
Profesa. Makame Mbarawa (kulia) akikagua mradi wa maji kwa Tom, Karatu Mjini.
Naye Mkuu wa wilaya ya Karatu Mhe. Theresia Mahongo amemshukuru Mhe. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli kwa kutoa fedha kwa ajili ya miradi ya maji. Mhe. Mahongo amemshukuru pia Waziri wa Maji Profesa Makame Mbarawa kwa kuja kuona changamoto ya maji wilayani Karatu. Amesema miradi minne ambayo fedha inakuja mwezi huu, itasimamiwa na watendaji wa maji badala ya wakandarasi wa maji hivyo miradi itatekelezwa haraka mpaka mwezi wa saba mwaka huu huduma za maji zitaanza kupatikana. Mhe. Mahongo amememuahidi Waziri wa Maji Profesa Mbarawa, kwamba yeye pamoja na wajumbe wa kamati ya ulinzi na usalama watailinda miundo mbinu ya maji. Mhe. Mahongo ametoa wito kwa wananchi kuendelea kutunza miundo mbinu ya maji.
Mkurugenzi mtendaji wa Halmashauri ya Karatu; Ndugu Waziri Mourice amesema, maeneo vilipochimbwa visima vya Ayalabe yalikuwa ni maeneo ya watu. Wenye maeneo waliridhia kabla zoezi la uchimbaji wa maji, tayari wataalamu walishaenda kupima kuona ni eneo gani wataweka mipaka kwa ajili ya maji na eneo gani wananchi wataendalea kulitumia kwa ajili ya shughuli zao. Ndugu Mourice amemuhakikishia Mhe. Waziri Profesa Mbarawa eneo hilo halina tatizo.
Mhe Willy Qambalo, ameeleza kilio cha wananchi wa kata ya Kansay ambele ya Waziri wa Maji Professa Mbarawa kwamba wananchi hawaamini viongozi wao hasa wanapozungumzia kuhusu Maji. Ameongeza kusema mradi wa maji wa Kansay wamekuja viongozi wengi lakini bado tatizo limeendelea kuwa sugu, amesema kutokana na adha ya maji wananchi wa Kansay wanalazimika kwenda kutafuta maji katika maeneo ya Hifadhi za wanyamapori jambo ambalo ni hatari kwa usalama wa maisha yao.
Karatu District Council
Sanduku la Posta: P.O Box 190
Simu: +255 272970648
Simu ya Mkononi: 0754773947
Barua Pepe: ded@karatudc.go.tz
Haki Miliki @ 2017 Halmashauri ya Wilaya ya Karatu.Haki zote zimehifadhiwa