Wenyeviti wa kijiji na vitongoji waliochaguliwa na kupita bila kupinga kwenye uchaguzi wa serikali za mitaa wameapishwa. Zoezi la uapishaji viongozi hao limefanyika kwa muda wa siku mbili, ili waanze kutekeleza majukumu yao ya kazi.
Msimamizi wa uchaguzi wilayani Karatu Ndugu Pius Haule amesema uchaguzi wa serikali za mitaa uliomalizika ulifuata kanuni na miongozo iliyoweka. Amesema kutofuata kanuni hizo kulisababisha wagombea wengi kushindwa kutimiza mahitaji ya ujazajaji wa fomu. Amesema ilikuwa ni jukumu la vyama vyote vitano vilivyopewa kanuni na miongozo ya uchaguzi wa serikali za mitaa kufuata maelekezo kikamilifu. Dosari ndogo za ujazaji wa fomu ndizo zilizoengua wagombea wengi na kusababisha kukosa sifa wakati wa uchaguzi. Amesema vyama vya siasa vilipaswa kutoa elimu hiyo kwa wagombea wao ili kuepuka dosari zilizojitokeza.
NDUGU PIUS HAULE AKITOA MAELEKEZO WAKATI WA UJAZAJI WA FOMU ZA KIAPO
Ndugu Pius Haule amewaasa viongozi walioapishwa kuepuka migorogoro ya uongozi katika utendaji wa shughuli zao sehemu za kazi. Amesema isitokee Mwenyekiti wa kijiji anagombana na Mtendaji wa kijiji katika utekelezaji wao wa shughuli za serikali. Amewaomba watendaji wa vijiji kusimamia ukusanayaji wa mapato katika maeneo yao ili waweze kutekeleza miradi ya maendeleo.
Ndugu Haule amewaasa viongozi hao kujiepusha na vitendo vya rushwa katika kipindi chao cha uongozi. Kuna tatizo moja kati ya watendaji wa vijiji na wenyeviti wa kijiji katika ukusanyaji wa mapato. Amesema mtendaji wa kijiji ni Afisa mhasibu wa kijiji, yeye ndiye anakusanya fedha na atafanya matumizi ya kijiji kwa ridhaa ya uongozi wa kijiji. Amesema wenyeviti wa vijiji ni wasimamizi wa vijiji wanahakikisha mapato na matumizi ya kijiji yanasomwa kila robo ya mwaka. Amesema Mkurugenzi mtendaji wa Halmashauri ya Karatu ataandaa semina elekezi kwa wenyeviti ili kuwaelimisha mipaka yao ya uongozi katika kufanya kazi kwa pamoja na watendaji wa vijiji.
Hakimu mfawidhi wa wilaya Mhe. I.B Kuppa amesema ukila kiapo kwa kamishina wa kiapo kama Hakimu au wakili yeyote unajipa jukumu. Kiapo kinatoa nafasi kwa kiongozi yeyote aliyekula kiapo kuchukuliwa hatua za kisheria kama ataenda kinyume na masharti ya kiapo.
Naye Mwenyekiti wa kijiji cha kambi ya Simba ndugu Faustine Simon Lulu ambaye awali alikuwa mwenyekiti wa kitongoji, amesema atafuata utaratibu wa kisheria na kanuni za uendeshaji wa kijiji kwa kuunda kamati za kudumu ili kusiamamia maendeleo ya kijiji. Amesema kwa kushirikiana na Halmashauri ya kijiji wataongoza shughuli za uzalishaji, na atawatumikia wananchi na wanakijiji wa Kambi ya simba kwa misingi ya utawala bora. Ikumbukwe kwamba nafasi zote za wenyeviti zimechukuliwa na chama cha mapinduzi kwa kushinda sehemu zilizofanya uchaguzi na wagombea wake kupita bila kupigwa kwa maeneo ambayo hawakufanya uchaguzi.
WENYEVITI WAKIWA WAMENYANYUA MIKONO JUU IKIWA NI ISHARA YA KULA KIAPO MBELE KAMISHINA WA KIAPO
Karatu District Council
Sanduku la Posta: P.O Box 190
Simu: +255 272970648
Simu ya Mkononi: 0754773947
Barua Pepe: ded@karatudc.go.tz
Haki Miliki @ 2017 Halmashauri ya Wilaya ya Karatu.Haki zote zimehifadhiwa